Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumanne KM alihitimisha ziara ya siku sita ya kutembelea mataifa ya Uswidin, Denmark na Uswiss. Kabla ya hapo, alijumuika asubuhi kwenye majadiliano ya meza ya duru, yaliokusanyisha Wakuu wa Serikali kutoka Mataifa Wanachama na maofisa wakuu watendaji (CEOs) wa makampuni ya kibiashara, waliohudhuria mkutano wa Geneva wa Shirika la Kimataifa juu ya Mawasiliano ya Simu (ITU). Kwenye hotuba yake KM aliwasihi mameneja wa makampuni, kutumia uwezo wao kuwahamasisha viongozi wa serikali za kimataifa waonyeshe ujasiri katika kutumia teknolojiya ya mawasiliano ya kisasa (ICT) nchini mwao, mfumo utakaowasaidia pia kutatua mizozo inayoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa, utaratibu utaowasilisha ‘uchumi wa kijani\' wenye kutunza mazingira.

Msemaji wa KM ameripoti kwamba hivi sasa UM unatathminia hali ya usalama ya ofisi ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), katika Islamabad, Pakistan ambayo mapema wiki hii ilishambuliwa na bomu la kujitolea mhanga. Ukaguzi huu ukimalizika UM utaamua kama ofisi za WFP zinafaa kufunguliwa kuendeleza shughuli zake au la. Licha ya hayo, huduma za kugawa misaada ya kihali kwa wahamiaji wa ndani ya nchi katika Pakistan, bado zinaendelea kushuhugulikiwa na watumishi wa WFP pamoja na wafanyakazi wa mashirika wenzi yasio ya kiserikali.

KM Ban Ki-moon ameripotiwa na msemaji wake, Michele Montas, kuwa ana wasiwasi juu ya tukio la karibuni katika Guinea ambapo vikosi vya usalama vilishtumiwa kunajisi kimabavu waandamanaji wapinzani wanawake. UM umependekeza kufanyike uchunguzi rasmi juu ya tukio hili na kuhakikisha wakosa wanafikishwa mahkamani ili, hatimaye, kukomesha, halan, tabia ya kufanya makosa ya jinai bila kujali adhabu. KM alinakiliwa akisema jinai iliotukia Guinea dhidi ya wanawake ilikuwa "ni kitendo katili na cha kutisha kabisa".

Shirika la Kimataifa juu ya Mawasiliano ya Simu (ITU) limechapisha takwimu mpya kuhusu matumizi ya mfumo wa mawasiliano ya kisasa ulimwenguni. Takwimu zilithibitisha kwamba robo moja ya idadi ya watu duniani hivi sasa huwa inatumia mawasiliano ya intaneti na kompyuta zilizounganishwa na mtandao wa kimataifa. Kadhalika, ripoti ilibainisha kwamba robo tatu ya kaya za kimataifa pia zinamiliki televisheni. Halkadhalika, kuhusu taarifa ziada juu ya ripoti tunayoizungumzia, mkuu wa ITU, Hamadoun Touré aliwatahadharisha walimwengu ya kuwa hakuna hata nchi moja iliosalimika na shambulio dhidi ya mfumo wa mtandao wa intaneti, hasa ilivyokuwa tunaishi kwenye mazingira ambayo teknolojiya ya mawasiliano ya intaneti ni muhimu kabisa katika uendeshaji wa shughuli za biashara, fedha, matunzo ya afya, huduma za dharura, ugawaji wa chakula na kadhalika.