Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Tarehe ya leo ni Siku ya Makazi Bora Duniani. Mada ya mwaka huu ya siku hiyo ni ile inayosema "Maandalizi ya Miji Bora kwa Siku za Baadaye". Taadhima za 2009 zinafanyika kwenye mji mkuu wa Marekani wa Washington D.C., na ni mara ya kwanza kwa sherehe hizi kuadhimishwa katika taifa la Marekani.

Katika Mkutano wa 2009 juu ya Mawasiliano ya Kisasa, ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa juu ya Mawasiliano ya Simu (ITU) mjini Geneva, Mataifa Wanachama yalinasihiwa na KM Ban Ki-moon kwenye risala yake, kuidhinisha ule mradi utakaoziwezesha skuli, hasa katika nchi zinazoendelea, kupata uwezo wa kuwa na mtandao wa teknolojiya ya mawasiliano ya kisiku hizi (ICT), ambayo itawasaidia kukabiliana vizuri zaidi na moja ya matatizo hatari yanayosumbua sayari ya dunia yetu kwa sasa hivi, yaani lile tatizo la athari haribifu zinazochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa. Aliwaomba washiriki wa kwenye mkutano kubadilishana mawazo ya ubunifu yatakayowasilisha kile alichokiita ‘uchumi wa kijani' utakaodumisha hifadhi bora ya mazingira kimataifa. Aliwasihi wajumbe wa kwenye mkutano kushirikiana kwa pamoja, kutafuta taratibu za "kupunguza uharibifu wa mazingira na kupunguza umwagaji wa hewa chafu kwenye anga, na kuwataka waandae sera za kuzalisha ajira zitakazowakinga walimwengu na maafa ya kimaumbile na, hatimaye, kuimarisha hali bora ya maisha."

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limefanyisha warsha maalumu kwenye mji wa El-Fasher, kwa kundi la awali la polisi 70 kati ya 200 wa Serikali ya Sudan, juu ya shughuli za usalama na ulinzi kwa wakati wa uchaguzi wa taifa wa 2010. Polisi hawa, baada ya kuhitimu mafunzo yao wanatarajiwa kuilimisha wenziwao 7,000 ziada katika kipindi cha miezi minne ijayo. Kamishna wa Polisi wa UNAMID, Michael Fry kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya polisi aliwaambia maofisa wa Sudan kwamba "jukumu muhimu la polisi katika Darfur wakati wa uchaguzi ni kuwapatia raia Wadarfuri usalama, kwa kulingana na mahitaji ya sheria."

Ijumapili, Mohammed El-Baradei, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) alikuwa na mkutano na wakuu wa Serikali ya Iran, mjini Teheran, ambapo walijadiliana utaratibu wa kutumiwa na wataalamu wa shirika, kuchunguza kiwanda kipya cha kusafishia madini ya yuraniamu, ambacho kinamalizwa kujengwa hivi sasa kwenye mji wa Qom. Wachunguzi wa IAEA wanatarajiwa kuzuru kiwanda cha Qom tarehe 25 Oktoba 2009, kufuatia taarifa ya Serikali ya Iran juu ya kiwanda hicho, iliotangazwa rasmi 24 Septemba 2009.

Ripoti ya 2009 juu ya Maendeleo ya Wanadamu (HDR), iliotangazwa leo Ijumatatu, imeeleza ya kuwa uhamaji wa watu kutoka makwao na kuelekea mataifa ya kigeni, ni kitendo chenye uwezo mkubwa wa kuimarisha uhuru wa umma na kustawisha maisha bora kwa mamilioni ya watu katika sehemu mbalimbali za dunia. Uchunguzi huu mpya unapinga zile itikadi zinazoaminika na wengi ulimwenguni kuhusu athari zisio sawa za wahamiaji kwenye maeneo wanaoelekea na katika nchi walipotokea. Ripoti ilipendekeza vifurushi kadha kuhusu hatua za kuchukuliwa kimataifa kukabiliana na suala la uhamiaji, ikijumlisha idhini itakayowaruhusu wafanyakazi kuingia kwenye nchi za kigeni kutafuta ajira kuwa kama ni msaada wa maendeleo kwa nchi zao, na kuwahakikishia haki za kufanya kazi kuwa zinahishimiwa na taifa pokezi. Ripoti ya Maendeleo ya Wanadamu (HDR), huchapishwa kila mwaka na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) na hujumuisha matokeo ya utafiti unaoendelezwa na wataalamu huru walioidhaminiwa na shirika kuendeleza utafiti huo.