Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kimataifa ya Kutotumia Nguvu wala Mabavu

Siku ya Kimataifa ya Kutotumia Nguvu wala Mabavu

Hii leo UM unaadhimisha Siku ya Kimataifa Dhidi ya Matumizi ya Nguvu. Risala ya KM juu ya siku hii imetoa mwito maalumu unaoutaka umma wote wa kimataifa kuiadhimisha siku hiyo kwa kukumbushana urithi wa kimaadili wa Mahatma Gandhi ambaye aliwahimiza walimwengu kutatua mifarakano yao kwa taratibu za amani, zisiotumia nguvu, mabavu wala fujo.

Kwa kulingana na nasaha hiyo, kwenye risala yake KM aliangaza juu ya jitihadi za UM katika kukomesha matumizi ya mabavu, bidii ambazo alisema zinajitahidi kuwahamasisha walimwengu kuangamiza milele zile silaha za mauaji ya halaiki. Vile vile alisema mwito wa Gandhi umejumuishwa kwenye kazi za UM zenye kusisitiza juu ya wajibu wa wanadamu kukomesha vitendo haribifu vinavyodhuru mazingira. Halkadhalika, kwa kuambatana na siku hii, KM amewahimiza washiriki wote wa kimataifa kujiunga na ile kampeni ya UM ya Kukomesha Matumizi ya Nguvu na Udhalilishaji Dhidi ya Wanawake.