Mwanaharakati wa kuhifadhi mazingira ahimiza viongozi wa dunia kuharakisha mapatano ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa

2 Oktoba 2009

Ripoti ya wiki hii itazingatia fafanuzi za mwanaharakati mashuhuri wa Afrika Mashariki anayetetea hifadhi ya mazingira ulimwenguni, kwa madhumuni ya kunusuru maisha ya vizazi vya siku za baadaye. Mwanaharakati huyo ni Profesa Wangari Maathai, mzalendo wa Kenya.

Profesa Maathai ni mwanamazingira maarufu, anayetambulikana takriban katika ulimwengu mzima. Vile vile mwanaharakati huyu wa mazingira alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi zake muhimu. Hivi majuzi Bi Maathai alihudhuria kikao maalumu cha kihistoria, kilichofanyika kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York, ambapo viongozi wa kimataifa walishauriana kipamoja namna ya kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa zilizopamba katika ulimwengu kwa hivi sasa. Kwa mujibu wa ripoti za taasisi za kitaaluma za kimataifa, imethibitishwa kihakika kwamba mnamo kati ya karne ya hivi sasa, inabashiriwa watoto milioni 25 ziada watateswa na njaa sugu itakayotokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, tukio ambalo litazusha upungufu mkubwa wa chakula na kusababisha bei ya vyakula vikuu kama mchele, ngano, mahindi na maharagwe ya soya kupanda kwa kiwango ambacho watu wa kawaida watashindwa kukimudu. Kadhalika ripoti ilihadharisha kwamba pindi ongezeko la joto halitodhibitiwa kidharura na nchi wanachama wa UM, madhara yake yataenea katika sehemu zote za ulimwengu, zitaathiri zaidi kimaisha zile jamii ziliopo katika mataifa Asia ya kusini na nchi za Afrika kusini mwa Sahara. Kwa hivyo, kwenye hotuba alioiwakilisha mbele ya kikao cha Baraza Kuu juu ya udhibiti wa mabadiliko ya haliya hewa, Profesa Maathai aliwahimiza viongozi wa kimataifa na jamii ya umma wa ulimwengu kushirikiana kukabiliana na suala hili kwa ari ya pamoja itakayovua vizazi vya miaka ijayo na madhara ya kimazingira yanayohatarisha ustawi wa maisha, kwa ujumla.

Mtayarishaji vipindi wa Redio ya UM, AZR, alipata nafasi ya kuhojiana na Profesa Maathai, kwa kutumia njia ya simu, wakati alipokuwa anazuru Kanada. Alianza kwa kumwomba Profesa Maathai atupatie maoni yake ya jumla kuhusu matokeo ya kikao cha Baraza Kuu?

WM:  "Mimi niliona kwamba ilikuwa ni mkutano mzuri sana kwa

WM sababu viongozi wengi walikubali kwamba tuko na shida hii ya climate change na ni lazima tuungane tukiwa dunia ili tuweze kufanya linalohitajika huko Copenhagen.

AR:Na ulipohutubia mkutano, uliwahimiza viongozi wa dunia waharakishe mapatano yao kabla hawajakutana mwezi Disemba Copenhagen. Ulipendekeza mapatano yao yawe na lengo au tuseme nia ya kuleta mafanikio makubwa au kuwa na mapatano yenye nguvu ya sheria kutekelezwa. Tusaidie hapa kidogo kuchambua kauli hiyo, hasa ulikusudia nini, mchango wa aina gani ungependelea kupata kutoka viongozi wa dunia juu ya suala hili?

WM: Kwa kweli, kama tunavyoelewa mazungumzo haya yote ni juu ya viongozi wa kila nchi, na bila viongozi wa kila nchi kuona ya kwamba ni mambo ya muhimu na kutekeleza mambo hayo katika nchi yao, hata tukifika huko Copenhagen, hakuna ile inaweza kufanyika; kwa hivyo nilikuwa kwanza kabisa nikiuliza viongozi, yaani heads of state wakubali ya kwamba ni lazima tufanye kazi hii pamoja - tukiwa na wale tumeendelea, na wale bado tunajaribu kuendelea, na tuungane pamoja Copenhagen. Huyo ndio ulikuwa mwito wangu, na nilikuwa nikiongea kwa binafsi ya wananchi wa dunia, na kwa hivyo, nilikuwa nikisema nyinyi ni viongozi wetu na vile mtatuongoza ndivyo tutafuata. Msipotuongoza, hakuna kile tutafaulu Copenhagen. Huo ndio ndio mwito wangu.

AR: Lakini ikiwa viongozi bado hawakubali mapendekezo ya umma, au yale ya mashirika ya raia, ambayo ulikuwa unayawakilisha, ni njia gani ungelitumia kuwasukuma wao kufikia hisia za umma?

WM:Kwa kweli, kama unavyojua wananchi, kile wanaweza kufanya kwa viongozi wao ni kuwauliza wakubali yale wanaomba kwa sababu sasa hakuna ile ingine unaweza kutumia. Kwa sababu ile unaweza kufanya tu, ni kuongea na kusema, na kuwafanya wasikilize kama vile walinipatia hiyo nafasi ya kuongea, na hawa ili wakasiliza, na vile vile katika nchi yetu kuna wengine ambao tukirudi manyumbani kwetu kuna wale ambao wataweza kuongea na seneta wao, wataweza kuongea na representative wao, watataweza kuongea na MP wao na kuwaonyesha ya kwamba hii kazi ni muhimu sana, na watu wananchi katika dunia hiyo tu ndio wanaweza kufanya. Na sisi tukiwa kwetu tunajaribu kuongea na Prime Minister wetu, na President wetu na ma-MP wetu ili waweze kuweka nguvu, na kuweka makini sana katika mambo haya. Hayo tu ndio tunaweza kufanya tukiwa wananchi wa dunia. Mara ingine, tunaweza kufanya kama vile nilifanya tukiwa pamoja, halafu tunatawanyika, tunaenda nchi zetu tunaendelea hiyo kazi.

AR:Na ulipohutubia Baraza Kuu, mapokezi ya mapendekezo yako yalikuwaje miongoni mwa viongozi wa kimataifa?

WM: Sema hiyo mara ingine?

AR: Mapokezi ya mapendekezo yako uliotoa mbele ya Baraza Kuu, ulipohutubia, miongoni mwa viongozi wa kimataifa, yalikuwaje?

WM: Kwa kweli mara nyingi huwezi kujua katika UN, kwa sababu kila mtu anakupigia makofi na unafikiri amekusikia, amekubali na wewe, lakini huwezi kujua. Lakini kama ulivyosikiliza, ulisikia vile kiongozi wa Japan aliongea, kiongozi wa China alivyoongea, hata viongozi wetu kutoka Afrika, vile walivyoongea na vile President (Barack) Obama (wa Marekani) alivyoongea, inakuonyesha ya kwamba wanaungana na wewe au wanakubali na yale wananchi wa dunia wanauliza. Kwa hivyo, mimi naona kama walisikia, sasa ile ya muhimu ni kuona tukifika huko Copenhangen, tutakuwa tumekubaliana, tutapunguza greenhouse gases kwa kiasi gani. Hiyo ndio ile muhimu kabisa, na kuna wachache sana kama wale wa China na wa Japan ambao walisema. President Obama, kama unavyokumbuka, hakusema. Kwa hivyo, ninajua bado hiyo ni kadi iko kwa mfuko wake mpaka tufike Copenhagen.

AR: Wanasayansi, hasa wale wanaohusika na utunzaji wa mazingira, wamethibisha kihakika kwamba misitu inaanza kuangamia kwa sababu mbalimbali zinazoambatana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa watu wa kawaida, ambao huwa wanategemea mapato ya kuendesha maisha kutokana na shughuli za misitu, mfano kama kukata miti kwa mbao na kadhalika, miongoni mwa fungu hili la watu wa pato la chini, njia gani utatumia kuwailimisha kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi misitu kwa wanadamu?

WM: Kwa kweli kama unavyojua tumefanya kazi hii kwa miaka zaidi ya miaka thelathini. Na tumekuwa tukijaribu kuilimisha watu. Na ikiwa kabisa, hata kwetu Kenya, watu hawajailimika, mara nyingi unaona ni shida sana kuilimisha wananchi. Kwa sababu watu wengi wanafikiria leo, hawafikiri kesho. Lakini kile tunaweza kufanya ni kuendelea tu kusomesha, na wale ambao wanakataa kusomeshwa, watasomeshwa na ulimwengu wenyewe. Kama vile umeona huko kwetu watu wamekufa. Wanyama wamekufa, kumekuwa na njaa kubwa sana. Na wakati huu ndio watu walikuwa wakisema, hawa Wangari na Greenbelt Movement imekuwa ikitueleza mambo haya kwa miaka mingi sana na hatukusikia. Sasa nasikia mvua imekuja, na wengi sana watapoteza maisha yao,kwa sababu kutakuwa na mafuriko, kwa vile tulikuwa tukiwaambia ni lazima mpande miti, ni lazima mchimbe mitaro, ni lazima mtengeneze terraces, ni lazima mkate,cut off drain. Hakuna mtu anasikiliza. Basi tufanye nini? Ndio sababu ninaongea na wewe. Tunaendelea kuwauliza wananchi, jifundisheni wa jamani, tufanye mambo ya kusaidia mazingira, kwa sababu tusiposaidia mazingira na sisi wenyewe tutaangamia.

AR: Unaweza kuwaeleza wasikilizaji wetu, kama ulivyodokoza kwenye hotuba yako, kama kuna fungamano fulani baina ya demokrasia, utunzaji wa mazingira na utulivu na amani ya kitaifa na kimataifa? Ulikusudia nini ulivyosema hivi?

WM:Kwa kweli kama watu wengi wanajua ya kwamba vita vingi ambayo tunapigana, iwe ni huko kwetu Kenya, au ni Afrika, iwe ni ulimwengu, mara nyingi tunapigania mali ya asili, tunapigania mali. Kwa sababu sisi tuko wengi sana. Katika dunia tuko karibu bilioni 7. Na huko kwetu Kenya tumehesabiwa juzi tuko milioni 40. Na nchi yetu haipanuki, kwa hivyo tunaanza kupigania mashamba, tunapigania maji, tunapigania chakula, ni kwa sababu tuko wengi na mali haipanuki. Ndio sababu tunasema ya kwamba isipokuwa sisi tujifunza kutunza mali ile tunayo, ikiwa ni udongo, ikiwa ni misitu, ikiwa ni maji, ikiwa ni mito yetu, ili tuweze kujisaidia nayo, basi tutakuwa na shida nyingi sana kwa sababu tutaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe. Tutauana, kama vile tuliuana juzi katika huko kwetu Kenya, na juzi ingine watu walikuwa wanauana huko Rwanda, tunasikia huko Liberia, tunasikia huko Kongo, tunasikia Darfur. Vita hivi vingi sana ukiangalia watu wanapigania ardhi, wanapigania maji, wanapigania mahali ya kulima na mahali pa kujenga. Kwa hivyo, ndio sababu Norwegian Nobel Committee ikasema ya kwamba hii masomo ambayo ninajaribu kupeana through the Greenbelt Movement, ya kwamba ni lazima tupunguze vita katika dunia, kwa njia ya kutunza mazingira. Ni muhimu sana na ni mambo ya Afrika pekee au mambo ya upande mmoja wa dunia, ni mambo ambao ni ya dunia nzima. Na ndio sababu ninafurahi sana wakati nilipatiwa wakati niende huko UN niongee na dunia ili niseme kweli hii ni mambo itafuata kila watu. Lakini sisi watu wa Afrika hasa nikiongea na watu wa Afrika, ambao wanaelewa hiyo lugha ninaongea nayo kwa kweli sisi watu wa Afrika tutaangamia zaidi wa wote kwa sababu sisi, ingawa hatukuweka greenhouse gases kwa hewa, kila mwanasayansi anasema Afrika itakuwa na shida nyingi sana. Kwa hivyo, wajamaa ni watu wetu. Ni lazima tuamke, ni lazima tuamke.

AR: Na vipi mataifa wanachama wataweza kuchangia kusaidia nchi zilizo na uchumi mdogo, kuzuia kwa mafanikio, uharibifu unaoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa?

WM: Kuna mipango ambayo najua itatengenezwa ya kupata pesa ili pesa hizi ziweze kusaidia watu, upandaji wa miti, kusaidia watu kuchimba mashimo, kuchimba terraces, kuchimba mitaro, kama vile ninaeleza, ili kulinda maji na kulinda umomonyoko wa udongo usitokee, na vile vile kulinda misitu. Na kile mimi ningetaka kusema ni kwamba pesa zitakazokuja wajamani tuzitumie bila kuiba, bila uharibifu na kufanya kazi nayo. Kwa sababu tusipofanya hivyo, wale wanatupatia hawana makosa, ni sisi tutakuwa na makosa kwa sababu hatukufanya ile tulikuwa tumesema tutafanya. Ninajua, vile vile, dunia tunaiuliza itusaidie kulinda misitu yetu, tuiache ikisimama, tusikate, watupatie pesa ili tutumie hiyo pesa na mambo yale tulikuwa tukijaribu kutumia misitu nayo, ili iweze kutusaidia katika dunia, kwa kuchukua hiyo carbon dioxide na kuzuia isiendelee kuharibu mazingira. Lakini vile vile ni lazima ikiwa tumefanya commitment, ikiwa tumesema tutalinda misitu na tupatiwe hiyo pesa, ni lazima tulinde misitu. Tusije tukajulikana kama watu hawawezi kuaminika, tunapatiwa hiyo pesa na hatufanyi ile tulisema tutafanya nayo.

AR: Na kabla ya kumaliza, una nyongeza yoyote, itayowasaidia kuwafahamisha wasikilizaji wetu juu ya umuhimu wa kuwa na mapatano ya kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani?

WM: Basi mimi ningerudia tu bwana, ningerudia tu ile nimesema mara nyingi, ya kwamba mazingira haina haja na wale ambao wanakataa kufanya kazi nayo. Nasema kwa kimombo, ukiharibu environment, if you destroy the environment, the environment will destroy you. Na hii ni muhimu sana tujue kwa sababu environment si mtu ati mtakaa chini kusikilizana. Ukiharibu misitu, utakuta siku moja huna mvua, utakuta siku moja mimea yako katika shamba imekauka, na utakuta siku moja unakufa kwa njaa, na hiyo environment haijali, kwa sababu wewe hukutumia maarifa ambayo umepatiwa na Mungu utumie.

AR: Professor Maathai tunakushukuru kushiriki katika mahojiano haya na Redio ya UM, ahsante sana.

WM: Ahsante, nashukuru."

AWK: Huyo alikuwa Mtayarishaji vipindi vya Redio ya UM akizungumza na Profesa Wangari Maathai, mwanaharakati wa kuhifadhi mazingira, juu ya umuhimu wa kuwa na mapatano ya kimataifa kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Nikiripoti kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM, NY huyu ni AWK.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter