Hapa na pale

Hapa na pale

Baada ya wajumbe wa Baraza la Usalama kusikiliza taarifa ya Haile Menkerios, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa, Ijumatano, kuhusu fujo zilizozuka Guinea, walitoa taarifa maalumu iliobainisha wasiwasi wao kuhusu mauaji yaliofanyika tarehe 28 Septemba pale jeshi la Askari wa Guinea liliposhambulia kwa risasi, kwenye mji wa Conakry, raia na kuua watu wanaokadiriwa 150 na kujeruhi mamia wengineo. Ripoti zilisema wanajeshi vile vile walinajisi kimabavu wanawake, kweupe mchana, kwenye mitaa. Wajumbe wa Baraza la Usalama wamelaumu kwa kauli kali vitendo hivyo, na wakatui huo huo kuwahimiza wenye mamlaka kukomesha haraka fujo na vurugu nchini mwao, na kuhakikisha watawafikisha mahakamani wakosaji wa jinai ya kijinsiya. Kadhalika walinasihiwa kuwaachia kutoka vizuizini wafungwa wote wa kisiasa.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire, Young-Jin Choi ameiambia Redio ya UM ya kuwa matatizo ya kiufundi huenda yakachelewesha uchaguzi kufanyika kwenye ule muda maalumu ulioandaliwa hivi sasa, hali ambayo huenda ikaathiri vibaya utulivu. Alisema miezi miwili imeshapotea kwa sababu ya matatizo ya kiufundi. Lakini alikumbusha pia kwamba mafanikio kadha yamedhihiri nchini, hasa katika mifumo ya kisiasa ambapo, mathalan, kumeanzishwa kwa mahakama ya kusafiri, yenye uwezo wa kusikiliza kesi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi. Vile vile alisema usajili wa wapiga kura umeshakamilishwa kote nchini. Aliongeza kwamba mazingira ya kisiasa yaliojiri Cote d'Ivoire kwa sasa yanaashiria matumaini mazuri kuhusu uchaguzi ujao.

Ripoti alizopokea KM juu ya utekelezaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK) zinasema hali huko ni ya kutisha na inamtia wasiwasi mkubwa Ban Ki-moon, hususan zile ripoti zenye kuonyesha Serikali imeshindwa kuchukua hatua muhimu dhidi ya ukiukaji wa haki za kimsingi unaoendelezwa kwa mipangilio, hali ambayo pia huwakosesha raia husika ulinzi halali wa haki zao. KM pia alisumbuliwa na ripoti zinazosema misaada ya chakula iliokuwa ikitolewa na jumuiya ya kimataifa kwa DPRK imepunguzwa kwa kiwango kikubwa, juu ya kuwa mashirika yanayohusika na misaada ya kihali yameripoti mara kadha wa kadha kuhusu upungufu wa chakula nchini humo. KM, kwa upande wake, ameisihi DPRK kuupatia umma hifadhi wanayostahiki kuhusu haki zao za kibinadamu, na kujaribukuleta mageuzi yanayoridhisha kwenye sheria za nchi kwa uwiano unaolingana na majukumu waliodhaminiwa na mikataba ya kimataifa.

Vifusi vinavyoelea na kuzunguka nje ya eneo la dunia vimeripotiwa kuhatarisha matumizi ya anga yanayosarifika, kwa mujibu wa taarifa ya tahadhari iliotangazwa na Ofisi ya UM juu ya Masuala ya Angani (UNOOSA). Tatizo hili litajadiliwa, kwa kina, kimataifa wiki ijayo pale walimwengu watakapoadhimisha ‘Wiki ya Anga Nje ya Dunia'. UNOOSA imekadiria aina ya vifusi 300,000 vinazunguka Dunia hivi sasa, kwa kasi inayolingana na maelfu ya maili kwa saa, vifusi ambavyo vina uwezo na nguvu ya kuangusha, kuharibu na hata kuangamiza chombo cha anga. Wakati huo huo, katika anga nje ya dunia kuna satalaiti karibu 1,000 zinazozunguka sayari ya ulimwengu wetu, vyombo ambavyo hutusaidia kutupatia taarifa juu ya hali ya hewa, na hutumiwa kupima ramani, kuhudumia mawasiliano na shughuli nyengine za kimsingi.