30 Septemba 2009
Kamishna Mkuu wa UM kuhusu Haki za Binadamu, Navi Pillay ametoa mwito wa kubuniwa tume maalumu ya uchunguzi, itakayopelekwa Guinea, kutathminia ripoti inayoeleza Ijumatatu vikosi vya usalama vya Guinea viliua kihorera raia walioandamana mjini Conakry, waliowakilisha kundi la upinzani.
Pillay alisema licha ya kuwa wenye madaraka Guinea wameahidi kuwa watafanyisha uchunguzi wao wenyewe kuhusu tukio hilo, alisistiza kwamba ni muhimu kwa ukaguzi kama huo, kuwa ni huru na usiopendelea. Alisema mauaji ya umwagaji damu mkubwa uliofanyika Guinea usiruhusiwe kamwe kuwa ndio mfumo mpya unaotumiwa kuendeleza makosa ya uhalifu na jinai bila kuadhibiwa, hali ambayo alisema imeselelea nchini humo kwa miongo kadha.