Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagonjwa milioni nne wenye VVU wamefanikiwa sasa hivi kupatiwa tiba ya ART, kurefusha maisha

Wagonjwa milioni nne wenye VVU wamefanikiwa sasa hivi kupatiwa tiba ya ART, kurefusha maisha

Kuanzia mwisho wa 2008, watu milioni 4 wanaoishi kwenye nchi zenye pato la chini na la wastani, walioambukizwa virusi vya UKIMWI, walifanikiwa kupata zile dawa za matibabu za kurefusha maisha za ART. Jumla hii inawakilisha ongezeko la asilimia 36, kwa mwaka, la wagonjwa wanaotibiwa kwa dawa ya ART.

Taarifa hii ilibainishwa kwenye ripoti iliochapishwa bia na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) na Jumuiya ya Mashirika ya UM Dhidi ya VVU/UKIMWI (UNAIDS). Ripoti vile vile imeangaza mafanikio yaliopatikana katika kupima, kushauri na kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka mama mjamzito kwa mtoto. Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa WHO alisema ripoti imeonyesha kuwa katika kipindi cha karibuni, tumefanikiwa kupata maendeleo makubwa ya kutia moyo, kwenye zile jitihadi za kimataifa za kudhibiti UKIMWI, kwa kutumia tiba ya ART. Hata hivyo, Dktr Chan alihadharisha kwamba watu milioni 5 ziada wanaoishi na VVU duniani, bado hawana uwezo wa kufadhiliwa tiba hii na wala uwezo wa kupata uuguzaji unaofaa, na huduma kinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI pia zimeshindwa kuwafikia umma muhitaji, halkadhalika. Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya UM, eneo liliofaidika zaidi na tiba ya ART kurefusha maisha yalikuwa yale mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara.