Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raisi wa BK anatabiri 'enzi mpya ya uhusiano wa kimataifa' wakati wa kufunga majadiliano ya wawakilishi wote

Raisi wa BK anatabiri 'enzi mpya ya uhusiano wa kimataifa' wakati wa kufunga majadiliano ya wawakilishi wote

Ijumanne mchana Baraza Kuu la UM lilikamilisha wiki moja ya majadiliano ya mwaka ya wawakilishi wote, ambapo wajumbe kutoka nchi 192 walizungumza, ikijumlisha Wakuu wa Mataifa na Serikali 107, waliowasilisha hoja kadha juu ya sera za kuendeleza uhusiano wa kimataifa.

Wajumbe walisisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa inawajibika kuimarisha "usawa wa madaraka" miongoni mwa wanachama wote wa UM yenyewe, katika kukabili masuala yanayoutatanisha uliwengu wetu: kuanzia mifumo ya fedha ya dunia inayohitajia marekibisho ya kuridhisha, hadi maamirisho ya akiba maridhawa za chakula ili kuepukana na matatizo ya njaa, na walisisitiza pia ya kuwa wakati umewadia kwa Duru ya Doha ya mazungumzo ya biashara ya ulimwengu, iliochukua muda mrefu, kukamilishwa kwa suluhu inayoridhisha, hasa miongoni mwa nchi maskini; wakati walipendekeza ajenda ya kukomesha silaha za maangamizi irudiwe tena haraka kwa makusudio ya kuondosha wasiwasi uliotanda ulimwenguni kuhusu hatari ya kuenea kwa silaha hizi maututi. Mada hizo ni baadhi tu ya masuala yaliojadiliwa kwa nguvu na wajumbe wa kimataifa katika kikao cha 64 cha Baraza Kuu. Raisi wa Baraza Kuu, kwa mwaka huu, Ali Abdussalam Treki wa Libya, katika risala ya kufunga kikao, alisema alitiwa moyo sana kuona wajumbe waliohudhuria vikao kwenye ukumbi wa Baraza Kuu, na kwenye mikutano ya pembezoni na katika matukio kadha yaliofanyika Makao Makuu, "waliahidi upya kuendeleza ushirikiano wenye nguvu na wenye wahusika wengi" katika kusuluhisha mizozo ya kimataifa, mazingira ambayo alisema yamethibitisha uhusiano wa kimataifa kuingia kwenye "enzi mpya" katika kipindi cha hivi sasa. Alisema ushirikiano huu unamaanisha dhahiri kwamba kunatakikana "mfumo wa uhusiano wa kimataifa wenye haki na wa kidemokrasia, utakaoshirikisha, kwa usawa, Mataifa Wanachama huru" yote. Alitumai masilahi ya nchi masikini yatapewa umuhimu unaostahiki. Alisisitiza pia kwamba Baraza Kuu la UM ndio chombo pekee chenye uwezo wa kujumuisha juhudi za pamoja, za kuitatua mizozo ya kimataifa, kwa utaratibu utakaoleta suluhu yenye natija kwa wote. Alikumbusha Raisi wa Baraza Kuu umuhimu wa kuzingatia athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi ndogo za visiwa, ambazo zinahatarishwa kuangamia kwa sababu ya kufurika kwa kina cha bahari. Alisailia pia haja kuu ya kikanda na kimataifa kudhibiti mitafaruku inayoripuka katika nchi za Afrika na kuyakinga mataifa hayo na mizozo na vurugu. Alihadharisha kwamba mzoroto uliojiri kwa sasa, kwenye zile juhudi za kuutatua mzozo wa Mashariki ya Kati, hauwezi kusarifika milele bila ya suluhu, na angelipendelea kuona UM unashirikishwa zaidi kwenye juhudi hizo.