Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) limekaribisha amri ya utendaji iliotangazwa na Raisi Omar al-Bashir wa Sudan kusimamisha, haraka, zile sheria za ukaguzi na uchunguzi wa magazeti katika nchi. UNMIS iliripoti pindi uamuzi huo utatekelezwa utasaidia kuendeleza na kuimarisha mapendekezo ya Mapatano ya Amani ya Jumla (CPA) baina ya eneo la kaskazini na kusini, na kuandaa mazingira bora ya kutayarisha uchaguzi wa vyama vyingi uliopangwa kufanyika Aprili 2010.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, Kai Eide alipohutubia kikao cha hadhara cha Baraza la Usalama, kilichofanyika Ijumanne asubuhi, kuhusu hali katika Afghanistan alisema jumuiya ya kimataifa imefikia kipindi ambapo ni lazima kufanya maamuzi yenye natija za jumla kwa umma wa Afghanistan. Alionya kwamba kushikilia kurudia sera zile kwa zile zilizopitwa na wakati kutatua mzozo wa Afghanistan ni hatua isioweza kuleta natija yoyote kwa taifa hilo. Kadhalika, alieleza ya kuwa watu kadha, kutoka matabaka mbalimbali ya kitaifa, walikutikana kukiuka taratibu za sheria na kuendeleza vitendo vya udanganyifu katika upigaji kura, ikijumlisha maofisa waliosimamia uchaguzi, pamoja na wagombea uchaguzi na wafuasi wao, na hata maofisa wa serikali. Alisema wataalamu walioletwa kutoka nje wataendeleza ukaguzi juu ya viwango gani vya sheria vilikiukwa na baadaye kuthibitisha matokeo ya mwisho ya uchaguzi. Masanduku ya kura sasa hivi yatapelekwa Kabul kufanyiwa ukaguzi, kwa kulingana na sheria za kimataifa juu ya kadhia hiyo. Baada ya matokeo ya mwisho kuthibitishwa, alisema Mjumbe wa KM, maamuzi muhimu juu ya mshindi wa uraisi yatalazimika kutangazwa, na kuhakikisha wakati huo kunateuliwa serikali inayoaminika na yenye uwezo wa kuhamasisha umma. Aliongeza kusema anakubaliana na mwito uliotolewa mara kadha wa kadha wa kuitisha mkutano mpya wa kimataifa juu ya suala la Afghanistan. Alisisitiza kwamba pindi hali ya usalama itaruhusu angelipendelea kuona kikao hicho kitafanyika kwenye mji wa Kabul.

Baraza la Haki za Binadamu asubuhi limejadilia ripoti ya Tume ya Uchunguzi juu ya Mzozo wa Tarafa ya Ghaza, baada ya kusikiliza, awali, fafanuzi za ripoti kutoka mkuu wa Tume, Richard Goldstone, na vile vile kusikiliza taarifa za wawakilishi wa Falastina na Israel. Jaji Goldstone alinakiliwa akinasihi wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu kwamba "sasa ni wakati wa vitendo" dhidi ya ile tabia ya kufanya makosa ya jinai bila kukhofu adhabu, utamaduni muovu ulioselelea kwa muda mrefu katika eneo la Mashariki ya Kati, alitahadharisha. Hali ya ukosefu wa uwajibikaji, kwa wale walioshiriki kwenye makosa ya vita, na jinai dhidi ya utu katika eneo, alionya, imefikia kiwango kibaya kabisa kimaadili; ukosefu wa haki unaoendelea, alitilia mkazo, unadhoofisha matumaini ya kuwasilisha mfumo wa amani utakaoleta mafanikio kwenye eneo, hali ambayo kama haijadhibitiwa mapema, badala yake itachochea mazingira yenye kuendeleza na kukuza matumizi ya nguvu, fujo na vurugu. Tume ya Uchunguzi juu ya Ghaza ilifanya ukaguzi wa miezi mitatu kwenye eneo husika, na kufikia uamuzi ulioeleza kutendeka uvunjaji mkubwa wa sheria za haki za binadamu na sheria za kiutu uliofanywa na vikosi vya Israel kwenye operesheni zao za kivita katika Tarafa ya Ghaza, kwenye kipindi kilichoanzia tarehe 27 Disemba 2008 mpaka 18 Januari 2009, na kuongeza ya kuwa Israel pia ilitenda makosa yanayoyumkinika kutafsiriwa kuwa ni makosa ya vita, na jinai dhidi ya utu. Kadhalika, Tume iliamua makundi ya KiFalastina, yenye silaha, nayo pia yalifanya makosa ya vita, na huyumkinika yalitenda jinai dhidi ya utu. Ilivyokuwa Serikali ya Israel na wenye mamlaka kwenye maeneo ya WaFalastina hivi sasa wameshindwa kufanya uchunguzi unaoaminika juu ya madai ya ukiukaji sheria ulioelezwa na maamuzi ya Tume, Jaji Goldstone aliwaomba wawakilishi 47 wa Mataifa Wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu kuchukua hatua kadha za kuzingatia mapendekezo ya ripoti yao, ikijumlisha kupeleka ripoti ya Tume kwa Baraza la Usalama la UM.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay naye pia alizungumzia mbele ya Baraza la Haki za Binadamu Geneva, ambapo aliwakilisha ripoti yake ya muda, iliopendekezwa na wajumbe wa Baraza kwenye azimio S-9/1, iliopewa mada isemayo "Ukiukaji Uliovuka Mipaka wa Haki za Binadamu katika Maeneo ya WaFalastina Yaliokaliwa, hususan baada ya Mashambulio ya Karibuni ya Israel dhidi ya Tarafa ya Ghaza Iliokaliwa Kimabavu."

Ripoti ya karibuni ya KM juu ya Wanawake, Amani na Usalama, iliochapishwa rasmi siku ya leo, ilipendekeza kwa Mataifa Wachama, sio kulaani tu kwa kauli pekee uharamishaji wa haki za wanawake na watoto wa kike kwenye maeneo ya mapigano, bali vile vile yalitakiwa yachukue hatua za dharura kuwashtaki wale wote wanaokutikana kushiriki kwenye unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsiya. Alipendekeza kwa Baraza la Usalama kuandaa, kwa bidii zaidi, utaratibu utakaowahusisha wanawake kwenye mifumo yote inayoambatana na huduma za kulinda amani, hasa katika majadiliano ya upatanishi, na vile vile kwenye shughuli za utawala na ufufuaji wa huduma za uchumi na jamii baada ya mapigano kusitishwa.