Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID imelaani shambulio la Darfur Magharibi dhidi ya wafanyakazi raia na wanajeshi

UNAMID imelaani shambulio la Darfur Magharibi dhidi ya wafanyakazi raia na wanajeshi

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limelaani vikali shambulio dhidi ya moja ya msafara wao wa ulinzi, liliotukia Ijumatatu usiku kwenye mji wa El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi na kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa ulinzi amani.

UNAMID imeisihi Serikali ya Sudan kufanya kila iwezalo kuhakikisha waliohusika na tukio hili wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kushtakiwa. Taarifa ya UNAMID ilisema msafara wao ulikuwa umechukua wafanyakazi raia na wanajeshi na ulishambuliwa na watu sita mpaka wanane, waliokuwa wamechukua silaha. Ripoti za awali zinasema majambazi wenye silaha walishambulia gari tatu za UNAMID, bila ya maonyo, na kuiba moja ya magari hayo. Wanajeshi watatu walijeruhiwa ambao, baadaye, walipelekwa kwenye hospitali ya El Geneina kwa matibabu, na kufuatia hapo walihamishwa kwa helikopta na kupelekwa hospitali ya UNAMID iliopo Nyala, Darfur Kusini, kilomita 300 kutoka El Geneina. Ripoti za UNAMID zimeeleza watu waliodhurika na tukio hili walijumlisha wafanyakazi wa kiraia wa Sudan pamoja na wale wa kimataifa 5, pamoja na watu wawili wasiofanyakazi na UNAMID, na pia wanajeshi wa UNAMID 13 wakichanganyika na polisi 4. UNAMID ilikumbusha tena kwamba wahudumia shughuli za amani katika Darfur wapo kwenye eneo hili la Sudan magharibi kwa mintarafu ya kurudisha utulivu na amani ya eneo la mgogoro. Kwa hivyo, ilieleza UNAMID, shambulio lolote lile dhidi ya walinzi amani wake, humaanisha shambulio dhidi ya amani ya eneo, kwa ujumla.