Namibia kuyasihi Mataifa Wanachama kupitisha hatua kali dhidi ya serikali zinazochukua madaraka kimabavu

Namibia kuyasihi Mataifa Wanachama kupitisha hatua kali dhidi ya serikali zinazochukua madaraka kimabavu

Majadiliano ya wawakilishi wote bado yanaendelea kwenye ukumbi wa Baraza Kuu na yameingia siku ya sita hii leo.

Miongoni mwa wazungumzaji kutoka Afrika waliowakilisha hoja zao mbele ya wawakilishi wa kimataifa waliokusanyika kwenye kikao hicho, alikuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Namibia, Marco Hausiku ambaye Ijumatatu aliyahimiza Mataifa Wanachama kuafikiana kutoruhusu zile Serikali zilizoingia madarakani kwa kufanya mapinduzi, nje ya katiba, kushiriki kwenye shughuli za taasisi za UM, kwa sababu vitendo vyao havilingani na mfumo wa kidemokrasia. Aliyataka Mataifa Wanachama 192 kupitisha "azimio la dharura" litakalopiga marufuku serikali zisioteuliwa kwa kura, kushiriki kwenye shughuli za UM, kwa ujumla. Alinasihi pia kwamba UM unahitajika "kuunga mkono, kwa ukamilifu, msimamo wa kimaadili wa Umoja wa Afrika wa kutozitambua zile serikali zilizochukua madaraka kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi." Kwa kulingana na mapendekezo hayo, kwenye kikao cha wawakilishi wote Ijumaa iliopita, Baraza Kuu lilipiga kura kutouruhusu ujumbe wa Bukini kuhutubia mkutano, kwa sababu waliwakilisha lile kundi liliopindua serikali halali ya raisi wa taifa hilo aliyeondoshwa kimabavu madarakani kwenye mapinduzi mwanzo wa mwaka.