Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Tume ya Kuchunguza Ukweli juu ya Mzozo wa Tarafa ya Ghaza inatazamiwa kuwakilisha ripoti ya matokeo ya ziara ya uchunguzi wao, mbele ya wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu, Ijumanne asubuhi, mjini Geneva. Ripoti itawakilishwa na kiongozi wa tume, Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini. Wajumbe watatu wengine wa tume wataungana na Jaji Goldstone kuwasilisha ripoti yao, ikijumlisha Bi Hina Jilani, Profesa Christine Chinkin na Kanali Desmond Travers. Kadhalika, Baraza la Haki za Binadamu litasikia ripoti nyengine juu ya Ghaza kutoka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay, ikifuatiwa na taarifa za wawakilishi wa Falastina na Israel. Mswada wa azimio la kikaohicho umeshatayarishwa na Baraza la Haki za Binadamu, na utazingatiwa kupitishwa Alkhamisi au Ijumaa.

Ijumanne Baraza la Usalama litakutana kuzingatia ripoti juu ya shughuli na kazi za Shirika la Usaidizi Amani la UM katika Afghanistan (UNAMA). Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, Kai Eide, atawakilisha ripoti kwenye Baraza la Usalama. Kadhalika, Baraza la Usalama litafanyisha kikao cha hadhi ya mawaziri, siku ya kesho, kusailia hali katika Cote d'Ivoire. Yoon-jin Choi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire naye pia atahudhuria mkusanyiko huo.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika Cote d'Ivoire (UNOCI) limeripotiwa kuanzisha hivi sasa huduma za kupeleka vifaa vya kufanyia uchaguzi katika sehemu kadha za nchi ili kutayarisha upigaji kura karibu na mwisho wa mwaka. Asubuhi watumishi wa UNOCI walisimamia uhamisho wa vifaa vya kupiga kura, kutoka bandari ya Abidjan, ambavyo vilipelekwa kwenye ghala za Kamisheni Huru ya Uchaguzi. Fungu hili la awali la vifaa vya uchaguzi limepelekwa kwenye sehemu za mashariki na kusini, na mnamo mwezi mosi Oktoba vifaa ziada vya upigaji kura vitahamishiwa jimbo la kati na kwenye mji mkuu wa Yamoussoukro. Mpaka sasa hakuna mabadiliko juu ya tarehe ilioandaliwa uchaguzi mkuu kufanyika katika Cote d'Ivoire ambayo ni tarehe 29 Novemba 2009.

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limetoa ombi jengine lenye kunasihi kuachiwa huru wafanayakazi wake wawili waliotekwa nyara kutoka nyumbani mwao na maharamia, walioshikia bunduki, katika siku 35 zilizopita, katika Darfur Magharibi. UNAMID ilisema Serikali ya Sudan vile vile imo mbioni kujitahidi kuwatafuta watumishi wa taasisi ya kulinda amani Darfur walionyakuliwa na majangili. Wakati huo huo, washauri wa polisi wa UNAMID waliongoza mafunzo maalumu kwenye kambi ya wahamiaji wa ndani ya Duma, kuhusu kazi za polisi katika jamii za kiraia. Wakazi karibu 100 wa kwenye kambi hiyo walishiriki kwenye mafunzo yaliohusika na taratibu za kutekeleza sheria za kimsingi, haki za kibinadamu na kanuni za usalama wa kambini mwao, washiriki ambao walijumlisha viongozi wa kidini na wanawake karibu 30.

Wajumbe wa kimataifa wa hadhi ya juu wamekusanyika hivi sasa kwenye Kikao cha Tisa cha Mkutano wa Makundi Yalioidhinisha Mkataba wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa, unaofanyika Buenos Aires, Argentina. Risala ya KM iliyotumwa mkutanoni imeyahimiza mataifa kukamilisha maafikiano ya kuridhisha ilivyokuwa tatizo la kuenea kwa jangwa linahatarisha maeneo mengi ya dunia na linatakiwa kudhibitiwa kwa mchango wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa. Risala ya KM ilionya ya kuwa tatizo la kupanuka kwa jangwa huunyima umma husika fursa ya kutafuta rizki na kuukaba utamaduni wao kimaisha. Alikumbusha watu bilioni 2 wenye kuishi kwenye maeneo yaliokauka vilevile ni miongoni mwa umma wa dunia ulio dhaifu sana na masikini, na mara nyingi hukosa uwezo wa kumudu kamwe maafa haya ya kimaumbile. Alisema kilichobakia ni kwa jamii ya kimataifa kujirekibisha kwa taratibu zitakazolingana na mageuzi ya hali ya hewa.

Grégoire Ndahimana, alioshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) leo amekana kosa la kushiriki kwenye mauaji ya halaiki katika 1994. Ndahimana alikuwa mtoro tangu Juni 2001 pale aliposhtakiwa rasmi na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya ICTR, alitiwa mbaroni mwezi Agosti mwaka huu baada ya kufanyika operesheni za pamoja za vikosi vya MONUC na majeshi ya Serikali kwenye jimbo la Kivu Kaskazini, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK). Mshtakiwa alihamishwa kwenye Mahakama ya ICTR wiki iliopita. Kwa mujibu wa ICTR, Ndahimana aliwatega raia wenye asili ya KiTutsi kwa kuwashawishi kuingia kanisani kupata hifadhi kwenye mji wa Kivumu mnamo Aprili 1994, na baada ya hapo aliyahamasisha makundi ya majangili na kuwapa fursa huru ya kuua na kuchinja chinja umma uliojificha kanisani. Kadhalika Mahakama leo asubuhi ilisikiliza ushahidi mwengine, uliotolewa kwa mdomo, kuhusu kesi ya rufaa ya Protais Zigiranyirazo, ambaye mwezi Dsiemba 2008 alipatikana na hatia ya kushiriki kwenye mauaji ya halaiki Rwanda katika 1994. Mshtakiwa huyu alikuwa mbunge wa cheo cha juu, na ni shemeji wa marehemu raisi wa Rwanda Juvenal Habyarimama.