Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti juu ya Ushirikiano wa Viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria (ALMA)

Ripoti juu ya Ushirikiano wa Viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria (ALMA)

Kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu la UM, ambacho ni cha 64, kilianza rasmi wiki hii kwenye Makao Makuu. Viongozi wa Mataifa na Serikali zaidi ya 120 walikusanyika mjini New York kuhudhuria mikutano mbalimbali juu ya shughuli za usalama, amani, haki za binadamu, huduma za maendeleo na kadhalika.

Kwenye pembe ya kikao cha wawakilishi wote katika Baraza Kuu, kulifanyika matukio mengine yanayofungamana na juhudi za kimataifa za kuyatekeleza baadhi ya yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs). Miongoni mwa matukio hayo ilijumlisha zile juihudi za kuzuia kabisa na kudhibiti bora miripuko ya malaria na magonjwa mengine hatari.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa mwaka wa Baraza Kuu walijumuika kwenye tafrija maalumu ya kuanzisha mradi wa Ushirikiano wa Viongozi wa Afrika Kupambana na Malaria, mradi unaojulikana kwa umaarufu kama mradi wa ALMA ambao ulianzishwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akishirikiana na Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Udhibiti wa Malaria, Ray Chambers. Diane BAILEY mtayarishaji vipindi vya Kiingereza katika Redio ya UM alihudhuria tafrija hiyo na alipata fursa ya kuzungumza na Raisi Kikwete, ambaye alianza mazungumzo yao kwa kuelezea kwa nini viongozi wa KiAfrika wanahitajia kuchukua hatua hii ya pamoja kukomesha malaria:

"Leo tumefanya mkutano wa kuzindua ushirikiano,

ushirikiano wa viongozi wa Afrika katika mapambano dhidi ya 

malaria. Malaria ndio maradhi yanaoua watu wengi barani 

Afrika, ndio maradhi yanaoua watu wengi nchini Tanzania. 

Watu wanazungumza sana kuhusu UKIMWI, HIV and AIDS. Lakini maradhi yanaoua watu wengi sana Afrika na katika nchi zetu ni malaria. Lakini malaria ni maradhi ambayo tunaweza kuyaondoa kabisa, kwa sababu ziko nchi duniani ambazo zimefanikiwa kuondoa malaria. Marekani ni nchi mojawapo na nchi nyengine. Lakini vile vile hata sisi nyumbani, Zanzibar tumefanikiwa sasa kuondoa malaria, maradhi ambayo hayapo."

AWK: Raisi Kikwete aliendelea kwa kufahamisha taratibu zinazohitajika kuukomesha ugonjwa wa malaria kama ifuatavyo:

"Lakini malaria unayaondoa kwa kutumia nini? Kwa pale

kwetu sisi uzoefu umeonyesha kwamba wanafanya vitu vitatu.

Ya kwanza, ni kutumia dawa ya artemisinin (qinghaosu) ... dawa mseto ya artemisinin .. artemisinin ni combination therapy. Ya pili, ni kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa. Sasa zamani kulikuwa na vyandarua vilivyotiwa dawa, lakini ya muda mfupi. Sasa kuna vyandarua vilivyotiwa dawa ya muda mrefu. Unatia dawa kwa muda wa miaka mitano, na katika miaka mitano hivi vyandarua hivyo huhitaji tena kuweka dawa. Vyandarua ambavyo mbu akitua anakufa. Lakini mbu hawezi kumfikia mtu akamuuma akampa malaria. Ya tatu, ni kupulizia dawa, kupulizia dawa ndani ya nyumba, dawa ambazo zitaua mbu. Kwa hivyo, ukiyafanya haya matatu, na ndio yalifanyika kote duniani, unafika mahali ndio unaweza."

AWK: Raisi wa Tanzania alimaliza mahojiano kwa kufahamisha gharama zinazohitajika kulisaidia bara la Afrika katika kuzuia malaria:

 "Sasa yote haya ni ghali, ni ghali. Dawa hizi ambazo

unaweza... dawa mseto ni ghali. Jitihadi iliokuwepo duniani

kupitia kwa (Waqf wa) Rais (mstaafu wa Marekani, Bill) Clinton, Global Initiative ya Clinton, amezungumza na watengenezaji wa madawa, wamekubali kupunguza bei za madawa haya, ili serekali zetu ziweze, na serekali zetu zinaweza hasa kununua dawa kwa wingi na kuweza kuwatibia watu. Kwenye vyandarua, jitihadi ambao tunaifanya sasa pale kwetu sisi nchini, zaidi ni jitihada ya .. kwanza, ni kwamba hivi sasa tunatoa bure vyandarua kwa watoto wa chini ya miaka mitano. Lakini pia kwa kina mama wajawazito, vyandarua vile vimepewa ruzuku, bei ni chini, bei ni dola kumi lakini wagonjwa wanauziwa kwa shilingi mia tano sasa hivi. Hiyo ni ya pali (???). Lakini sasa hivi tunakwenda na utaratibu wa mpango ambao tumefanya kwa ... Bwana Ray Chambers kwamba tunataka sasa mwaka ujao watu waweze kupata vyandarua. Kila kaya ipate vyandarua viwili, vilivyowekwa dawa ambayo inakaa kwa muda mrefu. Na pia ndio tuna program sasa ile ya kupulizia madawa ya kuua mbu, ambao ndio program ambayo sasa tunaendelea nayo. Sasa tumemaliza ... sasa hivi tunaanza kwa upande wa bara ndio tutafika .. ndio tuanze hiyo program na tunaanza kwenye mawilaya 27 ambazo ndio zina matatizo makubwa ya malaria, halafu tukitoka kwenye wilaya hizo ndio tunaendelea kwenye maeneo mengine katika nchi yetu."