Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) limetangaza leo kuwa linahitajia kupokea kutoka Iran taarifa zaidi, na ruhusa ya kuchunguza kiwanda cha fueli ya kusafishia madini ya yuraniamu, ambacho kinajengwa sasa hivi na Iran. Marc Vidricaire, msemaji wa IAEA aliripoti kwamba kwenye barua iliotumiwa taasisi yao na Iran, mnamo tarehe 21 Septemba 2009, ilielezwa kwamba Iran inajenga kiwanda kipya cha kutengenezea nishati na taarifa zaidi juu ya kadhia hiyo, zitatumiwa IAEA "katika muda mwafaka na kwa wakati upasao." Vidricaire alisema "IAEA imeiomba Iran kuwapatia, haraka iwezekanavyo, taarifa maalumu kuhusu ujenzi huu na kuwapatia wataalamu wa IAEA ruhusa ya kuzuru na kufanya ukaguzi wa kiwanda ili kuthibitisha kama ni salama kufanya shughuli zake." Aliongeza kusema Iran imeiarifu IAEA kwamba hakuna vifaa vya kinyuklia kwenye jengo la kiwanda kipya.

Wiki hii, wakulima na matajiri wa mashamba katika mji wa Hiniyyeh, Lebanon kusini wamerejeshewa ardhi salama yenye eneo la mita za mraba 7,500 baada ya Vikosi vya Muda vya UM Kulinda Amani Lebanon (UNIFIL) kufanikiwa kusafisha yale mabomu yaliotegwa ardhini kwenye sehemu hiyo ya nchi. Vikosi vya UNIFIL vinajihusisha kikamilifu na zile shughuli za kiutu ambazo huwasaidia raia kufyeka mabomu yaliotegwa ardhini, kwa ushirikiano na Taasisi ya Utendaji ya Lebanon Dhidi ya Mabomu Yaliotegwa. Juhudi hizi zimeziwezesha timu za UNIFIL katika kipindi cha hivi sasa kusafisha mabomu yaliotegwa katika eneo la jumla ya mita za mraba milioni 4.7, ambalo katika siku za nyuma lilitapakaa mabomu ya kutega. Timu za UNIFIL vile vile zilifanikiwa kuangamiza silaha na mabomu ya kutega 32,000 katika Lebanon kusini.

Taarifa mpya zilizokusanywa na Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kutoka vituo vinane vya ugawaji wa chakula kwenye mji mkuu wa Mogadishu, Usomali zimeonyesha kunahitajika msaada wa dharura wa lishe kwenye eneo hilo. Vituo vya WFP vilisajili wagonjwa wa lishe 700 na liliweza kuwatibu watoto wachanga 3,250, chini ya umri wa miaka mitano, pamoja na mama wajawazito na wale wanaonyonyesha ambao walikutana kusumbuliwa na tatizo la utapiamlo. Kwa sasa WFP inahudumia misaada ya chakula kwenye vituo ziada vya kulisha 190 ambavyo hutumiwa kuwapatia watoto 70,000 wanaosumbuliwa na utapiamlo nchini lishe bora.

KM ametangaza ombi maalumu linaloyataka mataifa wahisani na taasisi za kimataifa kuonyesha ukarimu wao pale watakapokutana mjini Brussels mnamo tarehe 02 Oktoba, na kuwataka wachangishe msaada maridhawa unaohitajika kuimarisha shughuli za Shirika la Ulinzi Amani la UM katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT). Mkutano wa Brussles umeandaliwa na MINURCAT, Serikali ya Chad na Kamisheni ya Ulaya na unatakiwa kuchangisha dola milioni 17 za kuhudumia misaada ya kiufundi na miundombinu ya kikosi maalumu cha polisi wa Chad cha Détachement Intégré de Sécurité, kikosi kitakachodhaminiwa majukumu ya kuwalinda na kuwapatia hifadhi wahamiaji wa nje na wale wageni waliopo kwenye makao ya muda katika sehemu za mpakani, kaskazini-mashariki ya Chad karibu na Sudan. MINURCAT imeripoti kuwa itahitajia pia dola milioni 4 zida kutumikia mradi wa kuimarisha sekta ya mahakama na magereza nchini Chad.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay leo amekaribisha tukio la kihistoria linalohusikana na zile juhudi za kukomesha mateso, baada ya taifa la 50 kuidhinisha mkataba wa UM juu ya suala hilo. Switzerland iliidhinisha Itifaki ya Hiyari ya Mkataba dhidi ya Mateso, kitendo kitakachoruhusu kuongeza wataalamu huru 15 watakaokuwa na dhamana ya kufuatilia utekelezaji wa Mkataba katika siku za baadaye, wataalamu ambao watapewa madaraka ziada, ikijumlisha haki ya kuzuru, bila ya kutangazwa au kupigiwa mbiu, vituo vya kufungia watu na kuyapatia mataifa ushauri juu ya namna ya kuanzisha bodi za kizalendo huru za kuzuia mateso. Mkataba wa UM dhidi ya Mateso, wenye kibwagizo ziada cha Itifaki ya Hiyari, ulipitishwa 1984 na kuidhinishwa na mataifa 146.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa taarifa yenye kukadiria makampuni ya madawa yataweza kutengeneza dozi bilioni 3 kila mwaka za dawa ya chanjo kinga dhidi ya homa ya mafua ya H1N1. Takwimu hii ni ya kiwango cha chini ya makadirio ya siku za nyuma kwa sababu imegundulikana dozi moja ya dawa hiyo ina nguvu ya kuwapatia kinga dhidi ya maambukizi watu wazima na watoto wakubwa kwa wakati mmoja.

Mashirika matano ya UM, yakijumlisha UNICEF, UNAIDS, UNFPA, UNIFEM na WHO, yanatarajiwa kushirikishwa kwenye mwelekeo mpya wa kupambana na athari za afya na ukiukaji wa haki za watoto wa kike wanaoelemewa na mateso ya kutumia mabavu dhidi yao. Mashirika haya ya UM yatajiunga kikazi na Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Maradhi (CDC) pamoja na sekta ya binafsi ya watoaji misaada ya kiutu, kwa kupitia Mradi wa Kimataifa wa Clinton (CGI). Kwa mujibu wa UNICEF wadau wa mradi watashirikiana kipamoja kuchangisha fedha za kupanua uchunguzi wa matumizi ya nguvu ya kijinsiya dhidi ya watoto wa kike katika mataifa yanayoendelea na katika zile nchi zinazofufuka kiuchumi. Vile vile wataanzisha utaratibu wa kiufundi utakaotumiwa kupunguza matukio ya vurugu la kijinsiya dhidi ya watoto wa kike na kuendeleza kampeni ya kuamsha hisia za umma juu ya suala hili.