Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

"Matatizo makubwa yataukabili ulimwengu mzima ikiwa tutashindwa kuusuluhisha mzozo wa Usomali". Onyo hili lilitolewa na Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe alipohutubia wiki hiii mkutano wa Kundi la Kimataifa la Mawasiliano juu ya Usomali (ICGS). Alisema taasisi za mpito ziliopo nchini kwa sasa hivi ndizo zenye fursa ya kurudisha tena hali ya utulivu na amani Usomali, hali ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu 1991. Aliongeza kwa kusema ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kufadhilia misaada hakika, na yenye maana, kwa Serikali ya Mpito Usomali ili ipate uwezo wa kuimarisha vyema utawala wake. Msaada wa kimataifa vile vile utaisaidia Serikali kuanzisha taasisi zitakazoshughulikia mahitaji ya umma na baadaye kuzalisha natija za amani. Pascoe aligutusha kwamba mashambulio ya wiki iliopita mjini Mogadishu kwenye Makao Makuu ya vikosi vya ulinzi amani vya Umoja wa Afrika, AMISOM, yanathibitisha dhahiri kuwepo haja kuu ya kujumuisha jumuiya ya kimataifa katika kuisaidia Serikali ya Mpito kudhibiti bora utawala nchini.

Imeripotiwa na Vikosi vya Shirika la Mchanganyiko la Uangalizi Amani la UM/UA kwa Darfur (UNAMID) kwamba wamepokea taarifa za "kushtusha sana" kuhusu idadi kubwa ya majeruhi wa kiraia kutokana na mapigano ya karibuni katika Darfur Kaskazini. UNAMID imeyaomba makundi yanayohasimiana karibu na mji wa Korma, yaani vikosi vya Serikali ya Sudan na makundi ya waasi, kusimamisha, halan, mapigano yao, hali ambayo inahatarisha zaidi maisha ya wenyeji raia na kuchafua zile huduma za kupeleka misaada ya kihali kwa umma muhitaji.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imehadharisha kwenye taarifa iliotolewa siku ya leo ya kwamba kutokana na hali mbaya ya upungufu wa misaada ya chakula kwa Ethiopia, kuna hatari ya operesheni za kugawa misaada ya chakula kwa umma kumalizika katika mwezi Septemba. Hivi sasa kunahitajika kidharura msaada wa dola milioni 37 kuhudumia chakula cha kunusuru maisha, mchango ambao utatumiwa kuanzia kipindi cha sasa mpaka mwezi Disemba. Kadhalika, kwa sababu ya mripuko wa maradhi ya kuharisha katika majimbo kadha ya Ethiopia, timu ya pamoja ya wataalamu inayojumlisha mashirika ya UM - mathalan, kama lile shirika linalosimamia maendeleo ya watoto, UNICEF, shirika la afya ya kimataifa, WHO na OCHA - yakichanganyika na watumishi wa Wizara ya Afya, imeelekea kwenye Jimbo la Amhara kutathminia hali halisi ya dharura iliozuka huko hivi sasa. Timu hiyo itajaribu kuhakikisha kuna matayarisho ya kuridhisha ili kukabiliana na tatizo hilo la afya na kuzuia maradhi yasienee kwenye sehemu wanazokusanyika watu kwa idadi kubwa, kama vile katika maskuli na kwenye tafrija za kijadi na zile za kidini.

Kwenye tafrija ya utiaji sahihi wa Itifaki ya Hiari ya Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Kitamaduni, Kijamii na Kiuchumi, tafrija iliofanyika kwenye Makao Makuu ya UM, New York, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu Navi Pillay aliwaambia wajumbe waliohudhuria shughuli hiyo kwamba utiaji sahihi wao ulikuwa ni miongoni mwa shughuli muhimu kabisa kwa mwaka huu, zinazohusu Uidhinishaji wa Mikataba ya UM. Itifaki ya Hiari ya Mkataba imekusudiwa hasa kuwasaidia wale watu au makundi yaliochoka kudai, kwa muda mrefu, haki nchini mwao, kutuma malalamiko yao kuzingatiwa na Kamati ya UM juu ya Haki za Kitamaduni, Kijamii na Kiuchumi na, baadaye, kutekelezewa haki zao halali kwa kulingana na kanuni za Mkataba.

Malipo ya faida inayotokana na uuzaji wa rikodi ya kuadhimisha Sikukuu ya Krismasi ya msanii maarufu wa Kimarekani, Bob Dylan, rikodi itakayoanza kuuzwa tarehe 12 Oktoba 2009, yatafadhiliwa kama ruzuku na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) na mwimbaji huyo. Mchango huu unabashiriwa utawapatia watoto wa skuli nusu milioni, wenye njaa, chakula katika sehemu mbalimbali za dunia. Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Josette Sheeran amemshukuru Bob Dylna kwa ukarimu wake. Alisema msaada wake umekuja katika kipindi kigumu ambapo njaa inaendelea kukithiri ulimwenguni na kuhatarisha maisha ya watu milioni 108 katika sehemu kadha wa kadha za dunia.

Ripoti mpya ya matokeo ya taaluma ya kisayansi, iliotangazwa wiki hii na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) imehadharisha kwamba athari za mabadiliko ya hali ya hewa zimeoenekana kujongelea kwa kasi sana, na kwa haraka katika ulimwengu, kushinda ilivyodhaniwa katika siku za nyuma. Ripoti ilieleza yale matabaka makubwa ya barafu pamoja na miamba ya barafu iliopo Kaskazini ya nchi Nchi ya Dunia (Akitiki) yameoenekana kuyayuka na kunyanyua kina cha bahari, na wakati huo huo kusababisha bahari kuathiriwa na sumu ya asidi. Mkurugenzi Mkuu wa UNEP, Achim Steiner alinakiliwa akizihimiza Serikali Wanachama kuharakisha maafikiao yao ya Copenhagen ili kuuvua ulimwengu wetu na athari haribifu na maututi zitakazochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Raisi Jakaya Mrisho Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alkhamisi jioni alishiriki kwenye majadiliano ya jumla ya kikao cha 64 cha Baraza Kuu la UM. Kwenye risala yake mbele ya wajumbe wa kimataifa alitoa mwito maalumu wa kupendekeza apatiwe msaada wa kukabiliana na "jukumu adhimu" la kuzalisha ajira kwa vijana. Alisema vijana wanajumuisha asilimia 37 ya idadi ya watu waliotimia umri wa kufanya kazi, na wakati huo huo hujumlisha asilimia 60 ya wasio na kazi. Alieleza katika baadhi ya mataifa ya Afrika, ambapo hukutikana idadi kubwa ya vijana, wanaokithiri kwa kasi kila kukicha kushinda maeno yote ya ulimwengu, kiwango cha vijana waliokosa ajira kinakadiriwa kufikia asilimia hata 80. Alikumbusha kwamba upanuzi wa soko la ajira barani humo haukufanikiwa kulingana sambamba na jumla ya vijana wanaoingia kwenye soko la kazi. Alionya kwamba tatizo hili ndilo linalowafanya baadhi ya vijana waliokosa matumaini ya maisha kuwa kile alichokiita kama "uchochezi wa petroli ya kuchoma moto magurudumu ya mizozo isiokwisha kuripuka barani humo mara kwa mara." Alisihi kwamba Afrika pekee, bila ya misaada ya kutoka jumuiya ya kimataifa, haitomudu kulitatua tatizo hili. Alibainisha pia kwenye hotuba yake, kwa fahari na kujivunia, kwamba sehemu kubwa ya bara la Afrika kwa sasa hivi inastarehea mazingira ya kuridhisha ya amani, ikijumliisha pia taifa jirani la Burundi ambalo kwa muda mrefu lilighumiwa na mtafaruku wa mapigano na vurugu lisiojuwa kikomo. Hali hiyo ilisababisha makumi elfu ya raia wao kuhamia Tanzania miaka ya nyuma kutafuta hifadhi. Alisema idadi kubwa ya wahamiaji hawa wa Burundi wameomba sasa wapatiwe uraia wa Tanzania, kadhia ambayo alisema inahitajia mchango adhimu kutoka UM kuitekeleza kwa ridhaa yenye natija kwa jamii yote husika.