Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majadiliano ya wawakilishi wote kwenye Baraza Kuu yameingia siku ya pili

Majadiliano ya wawakilishi wote kwenye Baraza Kuu yameingia siku ya pili

Majadiliano ya jumla, kwenye kikao cha wawakilishi wote katika Baraza Kuu la UM, leo yameingia siku ya pili.

Kiongozi wa Libya Muammar Al-Qadhafi, alipohutubia kikao cha ufunguzi Ijumatano, ambapo vile vile alizungumza kwa niaba ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, alisema majadiliano ya mwaka huu yanafanyika katika wakati ambapo ulimwengu umekabwa na matatizo aina kwa aina, yakijumlisha ile mizozo inayochochewa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, uchumi wa kimataifa unaoregarega na vile vile matatizo ya chakula ulimwenguni. Alikumbusha kwamba UM ulipobuniwa katika miaka ya nyuma, ulianzishwa na nchi chache tu, wakati fungu kubwa la Mataifa Wanachama halikuchangia katika ubunifu wa taasisi hii ya kimataifa. Alisema nchi haba zilizotayarisha Mkataba wa UM zilihakikisha kuwepo tofauti za kimsingi baina ya dibaji ya (utangulizi wa) Mkataba na vifungu vya sheria ya Mkataba. Dibaji ya Mkataba wa UM, aliongeza kusema kiongozi wa Libya ilisisitiza kwamba Mataifa Wanachama yote yana hadhi sawa katika UM, yakiwa mataifa makubwa au madogo. Kwa hivyo, alisisitiza, kwamba madaraka ya kura ya vito waliodhaminiwa nayo nchi tano wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama, dhamana hiyo ni haramu na inakwenda kinyume na mapendekezo ya utangulizi wa Mkataba. Alisema yeye haitambui wala haikubali haki ya kura ya vito iliopewa nchi chache wanachama wa Baraza la Usalama. Alieleza ya kuwa, kwa maoni yake binafsi, anahisi Baraza la Usalama halistahiki kutambuliwa hata kidogo kama ni taasisi ya kuimarisha amani ulimwenguni bali ni "Baraza la Utawala wa Vitisho", kwa kulingana na namna linavyotumia maazimio yake kukandamiza mataifa madogo wanachama. Alilalamika kwamba mfumo wa sasa wa Baraza la Usalama unahitajia mageuzi ya haraka kwenye uwanachama wake, ambapo wajumbe 15 wa kimataifa huwakilishwa kwenye Baraza. Alisisitiza tena kwamba mfumo wa kuzipatia kura ya vito nchi tano wanachama ni mfumo utakaoshindwa kuupatia umma wa kimataifa usalama au amani. Kuhusu Baraza Kuu la UM, kiongozi wa Libya alisema haoni faida ya kuwepo kwa taasisi hii kwa sababu anaamini BK limegeuzwa kuwa ni jukwaa la kutoa hotuba na baadaye kutoweka, na amelifananisha BK sawa na Kona ya Wazungumzaji katika Bustani ya Hyde Park iliopo London, Uingereza ambapo watu hukusanyika kujadiliana kwa mabishano ya kauli upepo, kauli ambazo hazina taathira zo zote kwa ulimwengu. Kadhalika, Al-Qadhafi, ambaye alizungumzia kwa niaba ya Umoja wa Afrika, alipendekeza kwa mataifa ya Afrika kulipwa fidia ya dola trilioni kwa sababu ya kushuhudia taathira mbaya ya ukoloni kwenye maeneo yao, hasa baada ya rasilmali na utajiri wao kutekwa nyara na wakoloni katika miaka ya nyuma.