Ukomeshaji wa uenezaji wa silaha za maangamizi watathminiwa na Baraza la Usalama

24 Septemba 2009

Baraza la Usalama leo asubuhi lilikutana kwenye kikao maalumu kuzingatia uzuiaji wa uenezaji wa silaha za kinyuklia na upunguzaji wa silaha za maangamizi ya halaiki.

KM Ban Ki-moon, kwenye hotuba yake mbele ya mkutano, alilihimiza Baraza la Usalama kujiambatisha na mwelekeo uliobainika kimataifa kwa hivi sasa, ambapo walimwengu wanapendelea kuona silaha za kinyuklia zitafyekwa milele duniani. Raisi wa Marekani Barack Obama alikuwa mwenyekiti wa majadiliano kwenye kikao hiki cha kihistoria cha Baraza la Usalama. KM alitumai mkutano utasaidia kuwapatia walimwengu "mwanzo mpya kwa usalama wa siku za baadaye." Kabla ya majadiliano kuanzishwa Baraza la Usalama lilipitisha, kwa kauli moja, azimio liliotoa mwito kwa yale mataifa, ambayo bado hayajaidhinisha Mkataba wa Uzuiaji wa Uenezaji wa Silaha za Kinyuklia (NPT), kuuridhia mkataba huo mapema iwezekanavyo ili kuupa hadhi itakayowakilisha ulimwengu mzima. Kadhalika azimio limeyataka Mataifa yote kujizuia, kwa kila njia, kufanya majaribio ya kuripua silaha za kinyuklia na kuyahimiza kuidhinisha na kuridhia Mkataba wa Jumla Unaopiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Kinyuklia (CTBT). Alisisitiza kwamba "ufyekaji wa silaha za kinyuklia ndio utaratibu pekee wa busara wenye uwezo wa kuimarisha usalama duniani." Mkataba wa CTBT umeshaidhinishwa na nchi 181 kwa sasa, lakini Mkataba huo haujaungwa mkono bado na serikali tisa muhimu, ikijumlisha zile zilizotangaza kuwa zinamiliki silaha za kinyuklia na zile zisiotangaza.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter