Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha 64 cha Baraza Kuu kufunguliwa rasmi

Kikao cha 64 cha Baraza Kuu kufunguliwa rasmi

Viongozi wa dunia 120 ziada, waliokusanyika kwenye Makao Makuu asubuhi ya leo, wameanza rasmi, majadiliano ya jumla ya kila mwaka, kwenye kikao cha wawakilishi wote katika ukumbi wa Baraza Kuu la UM, siku moja baada ya kumalizika Mkutano Mkuu juu ya mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

Miongoni mwa masuala muhimu yanayotarajiwa kuzingatiwa kwenye mijadala ya kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu, cha 64, inajumlisha tatizo la ugaidi na muongezeko wa umaskini unaochochewa na mzozo wa kifedha kwenye soko la kimataifa. Risala ya KM Ban Ki-moon kwenye majadiliano ya Baraza Kuu ilikumbusha kwamba matatizo yote magumu yaliokabili ulimwengu wetu, kwa sasa hivi - kuanzia mgogoro wa chakula, nishati, matatizo ya uchumi na janga la maradhi ya homa ya mafua - hayatoweza kusuluhishwa bila ya kuwashirikisha wahusika wengi. Alisema walimwengu wanautegemea UM kuwapatia jawabu za matatizo yaliokabili dunia, na aliongeza kusema kwamba wakati vile vile umewadia "kuwa na UM unaoridhisha, na unaoaminika, utakaochukua hatua halisi zenye natija kwa wote."