Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM ameikaribisha hatua iliochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Kideomkrasia ya Kongo, mnamo tarehe 20 Septemba, ya kumpeleka Grégoire Ndahimana kizuizini Tanzania, kwenye Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda. Ndahimana, raia wa Rwanda aliyekuwa na cheo cha juu kwenye kundi la waasi wa Rwanda la FDLR, alikamatwa na vikosi vya JKK mnamo tarehe 10 Agosti 2009 kwenye jimbo la mashariki ya nchi. Alikuwa miongoni mwa watoro 13 walioshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) kuharamisha sheria za kiutu za kimataifa nchini Rwanda katika 1994. Kutiwa mbaroni Ndahimana na uhamisho wake kwenye Mahakama ya ICTR ni vitendo vilivyosaidiwa kwa mchango wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC), baada ya kuitika ombi la wenye mamlaka nchini humo.

Kamati ya Mawasiliano ya Muda, inayoratibu na kusimamia misaada kwa umma wa KiFalastina, ilikutana Makao Makuu Ijumanne ambapo Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe aliwakilisha ujumbe maalumu mkutanoni, kutoka KM, uliobainisha kuridhika kwake na mafanikio yalioshuhudiwa katika miaka miwili iliopita miongoni mwa wenye Mamlaka wa Kifalastina walioonyesha maendeleo ya kutia moyo katika shughuli za usalama, uchumi, usimamizi wa fedha, mageuzi ya maeneo yao na uratibu wa mipango ya kuimarisha maendeleo. KM alisema kwenye risala yake kwamba UM upo tayari kuwasaidia wenye mamlaka wa KiFalastina kukamilisha ule mpango wa kujenga majengo ya taasisi mpya za kuendesha taifa.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti hali kwenye jimbo la Yemen kaskazini, la Sa'ada, bado ni ya kigeugeu na ya hatari, licha ya kutangazwa kusitishwa mapigano kwa wiki mbili kuadhimisha Siku Kuu ya Eid. Hii ni mara ya pili kwa makubaliano ya kusimamisha mapigano kutofuzu kuhisihimiwa na makundi yanayohasimiana. Mnamo mwisho wa wiki iliopita utulivu wastani uliripotiwa kurudi tena kwenye mji wa Sa'ada, kwa mujibu wa taarifa ya UNHCR, lakini si kitambo miripuko ya mapigano ilizuka tena upya katika sehemu kadha jirani za eneo husika. Katika kipindi ambapo mapigano yalipungua kidogo, shirika lisio la serikali linaloshirikiana na UNHCR lilifanikiwa kuhudumia misaada ya kihali kwa watu muhitaji 1,600 katika mji wa Sa'ada.

Naibu Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Charles Petrie, ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa wa kukuza zaidi zile jitihadi zao za kupandisha mbegu za kudumisha amani nchini Usomali. Aliyasema haya alipohudhuria maziko yaliofanyika Bujumbura, Ijumapili, ya maofisa na wanajeshi wa Burundi waliouawa kwenye shambulio la bomu la kujitoa mhanga, liliofanyika karibuni kwenye Makao Makuu ya vikosi vya ulinzi amani vya Umoja wa Afrika (AMISOM) kwenye mji wa Mogadishu. Hivi sasa upelelezi kamili unaendelezwa kutafuta sababu zilizozusha shambulio hili.

Shirika la UNHCR limeukaribisha uamuzi wa serikali ya Chad kuwahamisha wahamiaji wa Sudan 28,000 kutoka kambi ya Oure Cassoni, iliopo katika eneo la mgogoro la kaskazini-mashariki mpakani na Sudan. UNHCR iliiomba serikali ya Chad, kwa muda mrefu, kuwahamisha wahamiaji hawo kutoka eneo liliopo kilomita 7, karibu sana na mpaka wa Sudan, eneo ambalo lilikuwa ni taabu kulifikia na misaada ya kihali, na ni eneo liliokosa usalama. Sasa hivi UM na Chad wanatathminia eneo jipya la kuwapeleka wahamiaji hawo karibu na mji wa Bahai.

Gisele Bündchen, mwonyeshaji maarufu wa mitindo ya mavazi kutoka Brazil ameteuliwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) kuwa Mtetezi Mfadhili atakayesaidia kuhamasisha umma wa kimataifa kuchukua hatua hakika za kutunza na kuhifadhi mazingira yao. Vile vile Gisele atasaidia kuamsha hisia za walimwengu kuhusu hatari kuu inayokabili sayari yetu, ikijumuisha uharibifu wa mazingira na athari chafuzi zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.