Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumaa kumetolewa rasmi ripoti mpya ya KM juu ya watoto walionaswa kwenye mazingira ya mapigano nchini Burundi. Alisema kuanzia Agosti 2009 UM umethibitisha kutogundua tena watoto wa umri mdogo walioshirikishwa mapigano na majeshi ya mgambo katika Burundi. Alitilia mkazo kwenye ripoti kwamba jambo muhimu la kufanyika kwa sasa hivi ni kuhakikisha watoto wote waliohusikana na makundi yenye silaha katika siku za nyuma huwa wanajumuishwa kwenye kadhia za maisha ya kikawaida kwenye jamii zao. Ripoti imependekeza kuanzishwe mfumo mpya wa kuwalinda watoto, kwa ujumla, na hatari ya kuajiriwa kimabavu na makundi ya waasi. Vile vile KM alipendekeza ndani ya ripoti kwa Kundi la Kazi la Baraza la Usalama juu ya hifadhi ya watoto kwenye maeneo ya mapigano kuzuru Burundi katika miezi ijayo, ili kufuatilia maendeleo kwenye jitihadi za kutekeleza ile miradi ya kuwahifadhi watoto Burundi.

KM Ban Ki-moon amewaandikia viongozi wa kundi la G-20, ambao sasa hivi wanajiandaa kukusanyika kwenye mji wa Pittsburgh, Marekani, barua maalumu inayowahimiza kuzilinda nchi maskini wakati zinapitia kipindi cha mizozo ya kiuchumi na kifedha. Vile vile aliwaomba viongozi hawa wakamilishe ahadi walizotoa London mwezi Aprili 2009 za kuchangisha msaada wa dola trilioni 1.1, hususan lile fungu la kuhudumia maendeleo ya nchi masikini linalojumuisha dola bilioni 50. Alitarajia mwaka ujao mchango huu utafikia dola bilioni 155, kiwango kilichoahidiwa kuchangishwa kwa makusudio ya kupunguza umaskini - jumla ambayo pia ilitarajiwa kuweka kando dola bilioni 65 kufadhilia nchi za frika kukuza maendeleo yao ya kiuchumi na jamii. Kadhalika barua ya KM ilipendekeza kwa wanachama wa Kundi la G-20 kuharakisha misaada ya kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwenye mataifa yanayoendelea, na kuwataka waanzishe mfuko maalumu ambao itakapotimia 2020 utakakamilisha dola bilioni 250 kwa mwaka, fedha zitakazotumiwa kufadhilia huduma za kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.