Haki za wahamaji kwenye vizuizi vya idara za uhamiaji zinahitajia marekibisho, anasema Pillay

Haki za wahamaji kwenye vizuizi vya idara za uhamiaji zinahitajia marekibisho, anasema Pillay

Alkhamisi mjini Geneva, Baraza la Haki za Binadamu, kwenye pambizo za kikao chake cha mwaka, iliandaa warsha maalumu kuzingatia kwa kina, masuala yanayohusu haki za wahamiaji na wahamaji wanaowekwa kwenye vituo vya kufungia watu vya idara za uhamiaji, haki ambazo katika miaka ya karibuni zilionekana kukiukwa kihorera na mataifa pokezi ya wahamaji.

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa warsha alitahadharisha kwamba masaibu wanayopata wahamaji, hasa wale wanaojikuta katika hali isio ya kikawaida, kwenye mazingira ya kigeni, ni miongoni mwa matatizo magumu yaliokabili jumuiya za taasisi za kimataifa zinazohusika na haki za binadamu kwa hivi sasa:

 "Moja ya masuala yatakayopewa umuhimu na ofisi yangu Geneva katika kipindi cha miaka miwili ijayo ni lile suala la kuimarisha  haki za binadamu kwa wahamaji. Mwelekeo huu wa kazi za Ofisi ya Kamisheni ya Hazi za Binadamu unatarajiwa kuhakikisha huduma zinazohusika na udhibiti wa uhamiaji, kwenye mataifa pokezi, hautoharamisha haki za binadamu za wahamaji."

AZR: Haki za wahamaji wanaowekwa kwenye vituo vya kufungia vya idara za uhamiaji ni masuala yanayoshughulisha sana taasisi za kimataifa juu ya haki za binadamu, ikijumlisha Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu na mashirika mengineyo ya kimataifa. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay alisisitiza vifungo kama hivyo dhidi ya wahamaji humnyima mfungwa mhamaji haki za kimsingi maana anaamini hatua hiyo inakiuka mikataba ya sheria za kimataifa juu ya haki za binadamu, kama anavyoeleza hapa:

"Aidha, taasisi hizi za kimataifa zinapendelea kuwepo  usikivu madhubuti wa jumla kuhusu muktadha unaosababisha [ibid] vitendo hivyo kufanyika kwa urahisi kitaifa, ikijumlisha ule mtindo ulioenea katika siku za karibuni, wenye kutia wasiwasi, wa kutafsiri uhamiaji usio wa kikawaida kuwa ni kosa la jinai. Kuingia ndani ya nchi bila ya viza halali kisheria, au kukaa muda zaidi ya ruhusa ya viza ya mgeni, vitendo hivi ni mambo yanayovunja sheria za utawala lakini hayawezi kutafsiriwa kuwa ni kosa la uhalifu."

AZR: Mkurugenzi wa Miradi ya wahamaji aliyewakilisha Kamisheni ya Haki za Binadamu kutoka Australia, anayeitwa Vanessa Lesnie alieleza kwenye risala yake mbele ya wajumbe waliohudhuria warsha, kwamba kwa kulingana na matokeo ya uchunguzi wao juu ya siha ya wahamaji wanaowekwa kwenye vizuizi vya idara za uhamiaji za Australia kwa muda mrefu, ilionekana wahamaji hawa mara nyingi huathirika kimwili na kiakili kutokana na usumbufu wa kuwekwa kwenye mazingira yaliokosa hisia za kikawaida. Alikumbusha fungu linalodhurika zaidi na mazingira kama haya hasa huwa hasa ni watoto wadogo, wanawake na watu wazima. Alihadharisha kwamba pindi wafungwa wahamaji hawa wakirejeshwa nchi zao, kwa nguvu, hushindwa kuishi maisha ya kikawaida kwenye jamii zao. Kwa sababu ya bayana hii ndipo Australia iliamua kujihusisha, katika kipindi cha miaka mingi, kuhifadhi haki za wahamaji na wale wenye kuomba hifadhi ya kisiasa, na anaamini mwelekeo huu ndio wenye fursa ya kuhishimu utu na kuwapatia wahamaji maisha mapya yenye natija za muda mrefu kwa wao na pia kwa jamii zao mpya zinazowapokea.