Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumatano UM umewasilisha ripoti juu ya namna nchi wanachama zinavyotekeleza ahadi za kusaidia kuyakamilisha, kwa wakati, yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia yaliokusudiwa kupunguza umaskini kwa nusu kabla ya 2015. Ripoti imethibitisha serikali zipo nyuma sana katika kutimiza ahadi za msaada wa fedha za kuhudumia mataifa yanayoendelea kuibuka kutoka kwenye mazingira ya umaskini na kukabiliana na matatizo ya njaa na masuala kadha mengineyo ya kiuchumi na jamii. Ripoti yenye mada inayosema ‘Kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa kwenye huduma za Maendeleo katika Kipindi cha Mizozo\' ilitayarishwa na Tume Maalumu ya Kazi ya UM Kuziba Pengo la Utekelezaji wa Malengo ya MDGs. Ripoti imeangaza kwamba kuna pengo la dola bilioni 35 zilioahidiwa kuchangishwa kila mwaka na nchi zenye maendeleo ya viwandani, wanachama wa kundi la G8, kwenye mkutano mkuu uliofanyika 2005 katika Gleneagles, Uingereza. Vile vile ripoti ilisema kuna upungufu mkubwa wa dola bilioni 20 zilizoahidiwa kupatiwa mataifa ya Afrika kila mwaka ili yaweze kukabiliana na matatizo ya maendeleo. Naibu KM Asha-Rose Migiro aliwasilisha ripoti hiyo ya UM mbele ya waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu. Aliwaambia kwamba "walimwengu, katika siku za karibuni, tulifanikiwa kufanya maendeleo ya kutia moyo sana katika kuimarisha mashirikiano ya kimataifa juu ya shughuli za maendeleo ... katika kile kipindi kabla ya mizozo ya uchumi na kifedha kuripuka kwenye soko la kimataifa." NKM alihimiza kwamba tunachokihitajia kwa sasa hivi ni "msukumo tofauti mpya utakaosaidia kukabili vyema vitisho vinavyohatarisha natija za uchumi na jamii, natija zilizopatikana hivi sasa kwa jitihadi kuu kabisa."

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), wahamiaji Waburundi 50,000 wamesharejeshwa makwao hivi sasa kutoka Tanzania, ambako baadhi yao walikuwa wakiishi tangu 1972. Wahamiaji 5,000 ziada ambao bado wamesalia Tanzania kwa sasa hivi, wanatazamiwa kurudi Burundi katika miezi michache ijayo. Mwakilishi wa UNHCR katika Tanzania, Yacoub El Hillo alinakiliwa akisema "msaada wa kuwarejesha wahamiaji makwao Burundi, kwa khiyari, uliandaliwa na UNHCR, kwa ushirikiano na serikali za Tanzania na Burundi" na ulikusudiwa kusuluhisha, kwa mara ya mwisho, lile tatizo lilioselelea kwa muda mrefu la wahamiaji. Mhamiaji wa 50,000 kurejeshwa Burundi alikuwa ni mtoto mchanga wa miezi 11 anayeitwa Happines, ambaye alivuka mpaka Ijumapili iliopita na wazee wake, wakiwa miongoni mwa wahamiaji wa Burundi 496 waliorejeaa nchini mwao. Hatua hii ilisherehekewa rasmi kwenye tafrija ndogo iliofanyika katika makazi ya Katumba, ambapo wazee wa Happiness, walifadhiliwa baiskeli mpya kuwa zawadi ya mtoto. Wazee wa Happiness ni wakulima na waliozaliwa na kukuwa kwenye kambi za makazi ya muda Tanzania.

Rashid Khalikov, Mkurugenzi wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) Ijumanne alikamilisha ziara yake ya wiki moja Yemen. Alipokutana na wawakilishi wa jamii ya mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu kwenye mji wa Sana'a, alibainisha kwamba umaskini mkubwa uliotanda Yemen kaskazini pamoja na mapigano ya karibuni ni hali iliosababisha uwezo wa watu kukabiliana na matatizo haya kufika mwisho wa kikomo. Alisema alipozuru kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi aliona aila za watu waliohajiri mastakimu mikono mitupu na bila ya chochote. Aliongeza kwa kusema wahamiaji wa ndani 150,000 Yemen kaskazini wanahitajia haraka sasa hivi misaada yote ya msingi ili kunusuru maisha: ikijumlisha chakula, maji safi na salama, makazi ya muda na uangalizi wa afya. Alisema ukosefu wa maji safi ya kunywa kwenye eneo la mgogoro ni hali inayomtia wasiwasi sana. Kadhalika, Khalikov alieleza kuvunjika moyo kwamba ombi la kuchangisha msaada wa dharura unaohitajika kuhudumia kihali mzozo wa hivi sasa, liliotolewa tarehe 02 Septemba, bado halijajibiwa na wahisani wa kimataifa na UM umeshindwa kupokea hata senti nyekundu ya msaada huo.