Raisi mpya wa BK afungua kikao cha 64 kwa mwito wa kuleta mageuzi kwenye mfumo wa UM

16 Septemba 2009

Ijumanne alasiri, kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu (BK), yaani kikao cha 64, kilifunguliwa rasmi hapa Makao Makuu na Raisi mpya, Ali Treiki wa Libya, ambaye alirithi nafasi hiyo kutoka Raisi Miguel d\'Escoto wa Nicaragua, aliyemaliza muda wake mapema wiki hii.

Dktr Ali Treiki, kwenye hotuba yake ya ufunguzi, alitoa mwito uliosisitiza kwamba wakati umewadia kwa UM kufanyiwa marekibisho yanayoridhisha, hususan katika Baraza la Usalama ambapo alisema angelipendelea kuona uwakilishaji wake unajumlisha maeneo mbalimbali ya kijiografia. Alikumbusha kwamba bara la Afrika pekee hujumuisha Mataifa 53, na alivunjika moyo kuona kwamba hakuna hata nchi moja ya Afrika iliokuwa mjumbe wa kudumu kwenye Baraza la Usalama, nafasi ambayo imedhaminiwa mataifa ya Uchina, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani. Alisema Mataifa ya Amerika ya Latina/Kusini na Mataifa Madogo Madogo nayo pia yamenyimwa fursa ya kuwa na kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama, mataifa ambayo alikumbusha, yakijumuika na yale ya kutoka Afrika hujumlisha zaidi ya nusu ya idadi ya umma wa dunia. Alisema inastaajabisha kuona maazimio ya Baraza la Usalama, lenye wajumbe wanaowakilisha mataifa 15 tu, huwa na masharti halali kisheria wakati yale maazimio ya Baraza Kuu, panapowakilishwa Mataifa Wanachama 192, huwa hayana nguvu ya sheria ya kimataifa sawa na maazimio ya Baraza la Usalama. Alieleza kwamba jamii ya kimataifa inawajibika kuleta mageuzi thabiti kwenye Baraza Kuu la UM yatakaoipatia tasisi hii, inayowakilisha umma wa kimataifa, uhalali utakaohakikisha sauti yake inasikika na kuhishimiwa na maazimio yake yanatekelezwa kama inavyostahiki. Juu ya masuala yanayohusu ushusiano wa kimataifa, Raisi wa kikao cha 64 cha Baraza Kuu alitoa mwito uyatakayo mataifa kusuluhisha tofauti zao kwa mfumo wa mazungumzo na hali ya kufahamiana, badala ya ile tabia ya kulazimisha vikwazo, ambavyo anaamini havina natija zozote bali ni kuongeza uhasama na chuki, na uasi. Juu ya vitendo vya ugaidi, ambavyo alivilaani, Raisi Treiki alisistiza kwamba ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kuzingatia mizizi, sababu na vipengele vinavyochangisha vitendo hivyo kuzuka, hali ambayo alisema inajumlisha ugaidi unaoendelezwa na watu binafsi, makundi pamoja na Madola; na alitilia mkazo kwamba kwa maoni yake binafsi, ugaidi wa Dola ni mfumo katili zaidi. Aligusia pia suala la umma wa KiFalastina ambao alisema wana haki ya kurejea kwenye ardhi zao zilizotekwa na kukaliwa kimabavu, na vile vile haki ya kuwa huru, kwa kulingana na maazimio yaliopitishwa na UM ili, hatimaye, usalama na amani ya eneo irudishwe. Halkadhalika, Raisi wa Baraza Kuu aliyahimiza Mataifa Wanachama kuharakisha maafikiano yao juu ya Mkataba wa Kudhibiti Kipamoja Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani kabla ya Mkutano wa Copenhagen kufanyika mwezi Disemba mwaka huu; na vile vile alizihimiza nchi wanachama kutekeleza ahadi zao kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ya kupunguza ufukara na umaskini kwa nusu kabla ya 2015 katika mataifa yanayoendelea. Raisi mpya wa Baraza Kuu alipendekeza kuchukuliwe hatua za haraka kudhibiti vyema uenezaji wa silaha na kukomesha milele silaha za kinyuklia na zile za maangamizi ya halaiki ya umma.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter