Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

David Gressly, Mratibu wa Eneo la Sudan Kusini kwa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan (UNMIS) Ijumaa alizungumza na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu, kwa kupitia njia ya vidio, ambapo alieleza ya kuwa mashambulio ya kikatili yanayoendelezwa na kundi la waasi wa Uganda wa LRA pamoja na miripuko ya karibuni ya mapigano ya kikabila ni mambo yanayohatarisha usalama wa umma wa Sudan kusini. Alizungumzia kutoka Sudan kusini na alieleza wanajeshi wa mgambo wa LRA, ambao huteka nyara watoto wadogo na huwatumia kama wapiganaji na watumwa wa kikahaba, wameselelea na kuendelea kuongoza operesheni zao kwenye eneo la magharibi ya mbali ya Sudan kusini. Kwenye jimbo la Western Equatoria kundi la LRA linaendelea na kampeni zao za vitisho - ambapo huiba mali na kuvamia nyumba za watu, makanisa na vituo vya afya. Kadhalika, kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) waasi wa Uganda wa LRA wameonekana wakoiba vyakula, na kuua raia wasio hatia, na vile vile huwateka nyara watoto wadogo wa kike na kiume ambao huwalazimisha kuwatumikia kwa nji zinazoharamisha kabisa kanuni za kiutu na haki za mtoto. Gressly alitoa mfano wa uharibifu wa waasi wa LRA, ambao katika mwezi Agosti mwaka huu walishammbulia maeneo ya Western Equatoria na Central Equatoria na kuzusha tatizo kubwa la watu 80,000 ziada kung\'olewa mastakimu. Kuhusu mapigano miongoni mwa makabila ya Sudan kusini, Gressly alibainisha kwamba mara nyingi uhasama baina yao hutokana na mabishano ya mali - hususan ngo\'mbe, maji na ardhi. Alisisitiza kwamba suala la umiliki wa ardhi ni "tatizo kubwa linalohitajia suluhu ya kuridhisha miongoni mwa makabila ya eneo la kusini, au si hivyo fujo na vurugu zitaendelea kusababisha hali ya hatari na wasiwasi Sudan kusini."

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti hali ya chakula Usomali inatarajiwa kuharibika na kuwa mbaya zaidi hadi mwisho wa mwaka, hususan katika yale maeneo yaliodhuriwa na ukame. OCHA ilieleza vyanzo vya mapato na chakula kwa kaya za katika miji hufungamana zaidi na shughuli za biashara na soko la mifugo katika majimbo yalioathirika sana na ukame ya Hiraan, Galgaduud, Mudug, Nugaal, Sool, Sanaag na Togdheer. Hivi sasa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) linapanga miradi ya ugawaji ziada wa vyakula vya kunusuru maisha kwenye zile jamii zilizoumizwa zaidi na ukame. Lakini bado kuna matatizo katika upelekaji wa chakula kwenye maeneo husika kwa sababu ya kujiri kwa hali ya kigeugeu ya usalama na chakula kieneo, hali ambayo imeilazimisha WFP kusitisha ile miradi ya lishe bora kwa watoto na mama wajawazito katika vituo 12 viliopo kwenye majimbo matatu ya Usomali. Wiki iliopita WFP ilitoa ombi maalumu kwa wahisani wa kimataifa kuchangisha msaada wa dharura wa dola milioni 200 zinazohitajika kuhudumia chakula watu muhitaji milioni 3.76 - sawa na nusu ya idadi ya watu katika Usomali - ili kujiepusha na janga hatari la vifo vya utapiamlo.

KM Ban Ki-moon ameripotiwa kushtumu kitendo cha kurusha makombora mawili dhidi ya Israel kilichofanyika Septemba 11 (2009), kutokea eneo la Lebanon kusini. Ripoti za UM zinasema vikosi vya Israel vilijibisha mashambulio haya kwa mizinga dhidi ya eneo ambalo makombora yanadhaniwa yalitukia. Taarifa zinasema hakuna aliyejeruhiwa kwenye tukio hili. Vikosi vya Muda vya UM kwa Lebanon (UNIFIL), kwa ushirikiano wa karibu sana na Jeshi la Lebanon, kwa sasa wanaendeleza uchunguzi kutafuta sababu zilizochochea mabadilishano haya ya makombora na mizinga. KM aliyasihi makundi yote husika kujizuia na shauku za ulipaji kisasi na kuyataka yatekeleze kikamilifu mapendekezo ya azimio la Baraza la Usalama 1701 (2006) na kuhishimu maafikiano ya kusimamisha uhasama kati yao.

Utafiti mpya ulioendelezwa na wataalamu wanaoungwa mkono na Shirika la Afya Duniani (WHO), umeonyesha kwamba vyanzo vikubwa vya vifo kati ya vijana, baina ya umri wa miaka 10 mpaka 24, husababishwa na ajali za barabarani, ujauzito na uzazi, pamoja na ajali za kujiua, matumizi ya nguvu, virusi vya UKIMWI na maradhi ya UKIMWI pamoja na kifua kikuu (TB). Kwa mujibu wa ripoti, vijana karibu milioni tatu hufariki kila mwaka, na asilimia 97 ya vifo hivi hukutikana katika nchi maskini na katika zile nchi zenye maendeleo ya wastani.