Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Naibu KM wa UM juu ya Masuala ya Sheria, Patricia O\'Brien aliwaambia wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Ushauri juu ya Uendeshaji wa Sheria ya Kimataifa Kuhusu Jinai, uliofanyika Makao Makuu wiki hii (09-11 Septemba), ya kwamba kuanzishwa kwa Mahakama ya Kimataifa Juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) ilikuwa ni hatua ya kihistoria kwenye juhudi za kutekeleza kanuni za kiutu za kimataifa, na kuendeleza haki kwa kuhishimu sheria kote ulimwenguni. Risala iliwakilishwa kwa niaba ya KM, na ilisisitiza kazi za UM katika kuendeleza amani, maendeleo na haki za binadamu ni kadhia zinazofungamana kwa ukaribu zaidi na kazi za Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC). Risala ya KM ilisema UM inaipa umuhimu mkubwa lengo lake la kuimarisha ushirikiano bora na ICC.

Rashid Khalikov, Mkurugenzi wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Kiutu ya Dharura (OCHA) hivi sasa ameripotiwa akielekea Yemen ambapo anatarajiwa kufanya ziara ya kuchunguza ukweli kwenye yale maeneo wanamoishi raia waliolazimika kuhama makwao, kwa sababu ya mapigano ya karibuni yaliopamba kwenye eneo la kaskazini ya nchi. Vile vile Khalikov atakutana na maofisa wa serikali na wawakilishi wa makundi yanayohudumia misaada ya kiutu nchini, kwa lengo la kupata ufahamivu mzuri zaidi juu ya mzozo huo. Mgogoro ulioripuka karibuni kwenye Majimbo ya Sa'ada na Amran, Yemen kaskazini, ulisababaisha watu 150,000 kung'olewa makazi, kwa mujibu wa taarifa za OCHA. Umma huu unahitajia misaada ya dharura ya chakula, maji safi, na vifaa muhimu vya msingi kuhudumia shughuli za nyumbani, na pia unahitajia huduma za afya. Mnamo tarehe 02 Septemba, UM ulitangaza ombi maalumu la msaada wa dola milioni 23.7 unaotaka ifadhiliwe kutoka wahisani wa kimataifa ili kuhudumia kihali umma waathirika wa mzozo wa Yemen kwa kipindi cha miezi minne ijayo. Kwa mujibu wa OCHA ombi hilo bado halijatekelezwa na inakhofiwa kila mchnago wa kimataifa ukichelewa hali itaendelea kuwa mbaya zaidi Yemen kaskazini.

Shirika la UM Linalofarajia Misaada ya Kihali kwa WaFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) limetoa taarifa yenye kueleza kwamba ijapokuwa skuli zimefunguliwa wiki za karibuni takriban katika sehemu zote za ulimwengu, kwa bahati mbaya watoto wa KiFalastina katika kipindi hiki bado wanaendelea kuwekewa vikwazo na Israel kuhusu vifaa vya masomo. Taarifa ya UNRWA ilieleza kuwa iliekewa na wenye mamlaka Israel vizingiti aina kwa aina, vya kihistoria, vya muda mrefu ambavyo haviruhusu vifaa vya masomo, kama vitabu, karatasi za kuandikia na kadhalika kuingia katika eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza. UM umeripoti kuwa hatua hii ya Israel haieleweki, hasa ilivyokuwa miradi ya mafunzo katika skuli za UNRWA, hujumlisha pia yale masomo muhimu juu ya haki za binadamu pamoja na Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu, mada ambazo zinategemeza maadili ya kimataifa yanayotilia mkazo utaratibu wa watu kuvumiliana kitamaduni na kusuluhisha mizozo kwa amani.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) ikishirikiana na Serikali ya Kenya kwa sasa wameripotiwa kutayarisha mradi wa dharura, ili kukabiliana na mvua kali zinazoashiriwa kunyesha mwaka huu, baina ya miezi ya Oktoba hadi Disemba. Idara ya Upimaji wa Hali ya Hewa ya Kenya imehadharisha, hali ya hewa ya mfumo wa El Nino imekutikana kujiandaa kuvamia eneo hili la Afrika Mashariki. Katika miaka ya nyuma, mvua ya El Nino ilipopiga Kenya ilisababisha maafa ya kila aina, zilisambaratisha taratibu za kutafuta rizki, ziling'oa makazi raia, na watu walipoteza mali zao, na wakati huo huo kuharibu vibaya sana miundombinu na kusababisha vifo vya watu na mifugo, halkadhalika.

Imeripotiwa na OCHA watu 48,000 walioathiriwa na mafuriko katika Burkina Faso hivi sasa wamehamishiwa kwenye makazi ya muda, ya majengo ya umma, ikijumlisha maskuli na makanisa, hali ambayo imezusha matatizo ya usafi wa mazingira kwa wahamiaji hawa wa ndani ya nchi. Mashirika ya UM yameshaanza kufarajia misaada ya dharura kwa waathirika, ikijumuisha ugawaji wa chakula, vifaa vya matibabu, zana za kuekezea makazi ya muda, zana za huduma za afya na mahitaji mengineyo ya kihali. Uharibifu mkubwa wa mafuriko hayo umeshuhudiwa zaidi kwenye maeneo ya mji mkuu wa Ouagadougou na vitongoji vyake ambapo wakazi wenyeji walilazimika kupokea waathirika ziada wa mafuriko 40,000 na kuwapatia hifadhi.