Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM ahimiza uundaji wa serikali mpya ya mpito Bukini

KM ahimiza uundaji wa serikali mpya ya mpito Bukini

Taarifa ilitolewa Alkhamisi na Ofisi ya Msemaji wa KM juu ya suala la Bukini, imeeleza kwamba Ban Ki-moon ametoa mwito unaowahimiza wenye mamlaka nchini humo kufikia maafikiano ya haraka juu ya uundaji wa Serikali ya Muungano wa Taifa, kama ilivyoidhinishwa na Mapatano ya Kisiasa ya Maputo yaliofikiwa tarehe 09 Agosti mwaka huu.

 Alisisitiza ya kuwa hakuna mfumo mbadala wa kutatua mfarakano wao, isispokuwa kwa kutekeleza mapatano ya kisiasa kwenye kipindi cha mpito kwa ridhaa ya makundi yote husika katika Bukini. Aliyataka makundi yote katika sekta zote za jamii ya Bukini kuwa watulivu, ili kuruhusu suluhu ya amani ya mzozo wao kushika mizizi itakayonufaisha umma. Taarifa ya KM ilitilia mkazo kwamba itaendelea kujihusisha na kadhia za kurudisha amani nchini kwa kupitia Tume ya Upatanishi wa Pamoja kwa Bukini.