Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waitaka Israel kuruhusu vifaa kuingia Ghaza haraka kufufua huduma za maji

UM waitaka Israel kuruhusu vifaa kuingia Ghaza haraka kufufua huduma za maji

Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwenye Maeneo Yailokaliwa Kimabavu ya WaFalastina, Maxwell Gaylard - akijumuika na Jumuiya za Mashirika Yasio ya Kiserikali yanayoambatana na Mashirika ya Kimataifa juu ya Misaada ya Maendeleo - wametangaza leo hii taarifa maalumu yenye kuthibitisha kufanyika uharibifu mkubwa wa vifaa vya huduma za usafi na maji katika eneo la Tarafa ya Ghaza, hali ambayo inazidisha ugumu wa maisha kwa umma wa eneo hili na kuwanyima hadhi yao ya kiutu.

Mratibu wa Misaada ya Kiutu wa UM ametoa mwito kwa Israel kuchukua hatua za dharura kuhakikisha vifaa vya kufanyia matengenezo na ujenzi huwa vinaruhusiwa kuingizwa Ghaza ili kudhibiti mazingira ya usafi na huduma za maji kwa wakati huo. Kwa mujibu wa Gaylard wakazi 10,000 katika Ghaza wamenyimwa uwezo wa kufikia mitandao ya huduma za maji safi na slama. Kadhalika, asilimia 60 ya idadi ya watu Ghaza imeripotiwa kunyimwa uwezo wa kupata, kwa muda mrefu na kwa mfululizo, maji safi na salama.