Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM asihi Mkutano wa WCC3 kuharakisha maafikiano ya kudhibiti mageuzi ya hali ya hewa.

KM asihi Mkutano wa WCC3 kuharakisha maafikiano ya kudhibiti mageuzi ya hali ya hewa.

Wajumbe kadha wa kimataifa waliokusanyika Geneva, kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Tatu juu ya Hali ya Hewa (WCC3) walipata fursa ya kumsikiliza KM Ban Ki-moon akisihi, kwa bidii kuu, juu ya umuhimu wa mataifa kuhakarisha makubaliano ya mkataba mpya wa kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia.

Aliyasihi Mataifa Wanachama kuchukua hatua za dharura ili kujikinga na hatari ya "kutanda kwa maafa makubwa ya kiuchumi" katika siku zijazo, kwa sababu ya kunyanyuka kwa kina cha bahari. KM alionya kwenye hotuba yake kwamba bila ya mataifa kuchukua hatua za pamoja kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa, yanayoashiriwa kuzuka katika siku zijazo, kwa kufikia makubaliano ya kuridhisha, kuna hatari ya vizazi vijavyo kukabiliwa na mizozo ya maisha isio kifani. KM alibashiria matokeo pindi mataifa yatapwelewa kuchukua hatua za mapema za kudhibiti taathira za mabadiliko ya hali ya hewa, kama ifuatavyo: "Mwisho wa karne hii, kina cha bahari kinatrajiwa kunyanyuka baina ya nusu mita mpaka mita mbili na tusisahau watu milioni 60 sasa hivi tayari wanaishi katika maeneo ya mita moja ya usawa na bahari .. idadi ambayo mnamo mwisho wa karne ya 21 itaongezeka na kuzidi watu milioni 130 wanaoishi kando ya bahari. Umma huu hukutikana zaidi kwenye madelta ya mito mikuu katika Afrika na Asia .. na kwenye visiwa vya nyanda za chini." KM aliuliza kwenye hotuba yake kwamba raia wanaoishi kwenye miji ya mwambao nini watafanya dhoruba kuu zikianza kuzisukuma bahari ndani zaidi ya nchi? Alitaka kujua wapi umma huu utakimbilia? Aliuliza watu wa Asia ya Kusini, Asia ya Kusini-mashariki na Uchina wafanye nini pale akiba yao ya maji kutoka Milima ya Himalaya itakapokauka, maeneo ambayo, alitilia mkazo, huishi karibu nusu ya idadi ya watu wa dunia!? KM alisema vile vile kuwa ana wasiwasi mkuu juu ya wakulima wa Afrika, na kuuliza umma huu nini utafanya pindi mvua zitashindwa kunyesha au mafuriko yatakapogharikisha na kuangamiza mazao yao? KM alisema jawabu ya masuala hayo imo kwenye kile alichokiita "ukuwaji wa mazingira ya kijani" unaosarifika, na wenye ustawi utakaonufaisha umma wote wa kimataifa. Kwa hivyo KM aliwasihi wajumbe wa Mataifa Wanachama kuharakisha maafikiano yao juu ya waraka wa mkataba mpya wa kuzingatiwa kwenye Mkutano wa Copenhagen utakaofanyika mwezi Disemba mwaka huu, maafikiano ambayo yakitekelezwa alisema yatasaidia kuuvua umma na maafa ya kiuchumi na jamii kwa siku zijazo.