Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zahimizwa kutekeleza ahadi za kuwasaidia wanusurika wa mabomu yaliotegwa ardhini

Serikali zahimizwa kutekeleza ahadi za kuwasaidia wanusurika wa mabomu yaliotegwa ardhini

Ripoti mpya ya kufanikisha yenye mada isemayo "Sauti za Kutoka Ardhini" imebainisha kwamba licha ya kupatikana maendeleo katika kuangamiza akiba ya mabomu ya kutega ardhini, kutoka ghala mbalimbali, pamoja na kuziondosha silaha hizo, hata hivyo serikali za kimataifa bado zimeshindwa kutekeleza ahadi zao za kuwajumuisha waathirika wa silaha hizo kwenye maisha ya kawaida ya jamii zao.

Ripoti ilieleza kwamba miaka 10 baada ya Mkataba wa Kupiga Marufuku Mabomu ya Kutega Ardhini (MBT) kufanywa chombo cha sheria ya kimataifa, asilimia 67 ya watu walionusurika na ajali za mabomu yaliotegwa ardhini wanaamini serikali zao zimeshindwa kuwatimizia mahitaji yao ya kimsingi. Taarifa hii imetolewa siku moja kabla ya kufanyika Mkutano wa Pili wa Matayarisho katika Geneva, kuanzia tarehe 03 mpaka 04 Septemba, ambapo wajumbe kutoka nchi 150 watakutana kujadilia mradi wa utendaji wa upigaji marufuku mabomu ya kutegwa ardhini kwa miaka mitano ijayo.