Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumatano Naibu KM Asha-Rose Migiro alihutubia kikao cha pili cha Mkutano wa Mataifa Yalioidhinisha Mkataba juu ya Haki za Watu Walemavu uliofanyika kwenye Makao Makuu ya UM. Kwenye risala yake alisema Mkataba wa Watu Walemavu unajumlisha misingi imara ya kisheria inayotakikana kwenye zile bidii za kusukuma mbele haki za watu milioni 650 - wanawake, wanaume na watoto wanaoishi na ulemavu - kutoka sehemu zote za dunia na, hatimaye, kuwawezesha kushirikishwa na kujumuika kikamilifu kwenye maisha ya jamii zao. Naibu KM alisema inatia moyo kuona mataifa mengi yameshapitisha sheria mpya na sera kadha zinazolingana na mapendekezo ya Mkataba, mwelekeo ambao alisema utasaidia kutekeleza kanuni za Mkataba kwa ridhaa ya wahusika wote.

Jorge Sampãio, Mjumbe Maalumu wa KM Kukomesha Kifua Kikuu akiandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya za UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), Michel Sidibé walizuru Kituo cha Matibabu ya Jamii (Socio-Medical Centre) kiliopo kwenye mji wa Biryogo, Rwanda ambapo walijionea moja kwa moja namna mchanganyiko wa matibabu ya UKIMWI na kifua kikuu unavyotumiwa kupima wagonjwa na kuwauguza kwa uangalizi wa huduma zilizofungamana. Sidibé alinakiliwa akisema UM utaendelea kuisaidia Rwanda kwenye jitihadi za kukabiliana na majanga ya TB (kifua kikuu) na UKIMWI. Alisema mafanikio walioshuhudia Rwanda katika kukabiliana na maradhi ya UKIMWI na TB ni huduma za kupigiwa mfano kote barani Afrika.

Jamii ya mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu, kwa ushauri na Serikali ya Yemen, leo yameanzisha kampeni ya kutaka yafadhiliwe msaada wa dharura wa dola milioni 23.5 zitakazotumiwa kufarajia misaada ya kihali kwa ule umma uliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano ya karibuni baina ya vikosi vya Serikali ya Yemen na majeshi ya mgambo yenye silaha. Makadirio ya hivi sasa yanaashiria watu 150,000 walilazimishwa kuhama makwao Yemen kaskazini kwa sababu ya mapigano, ikijumuisha watu 95,000 waliofurushwa na mapigano ya siku za nyuma, pamoja na watu wengine 55,000 walioyahama makazi yao katika mwezi Julai. John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu, aliongoza kampeni ilioanzishwa Geneva inayowataka wahisani wa kimataifa kuisaidia Yemen kidharura kukabiliana na mzozo wa kihali uliokabili waathirika wa mapigano ya karibuni nchini. Alisema mkumbo wa karibuni, uliozusha ukosefu mkubwa wa makazi, umesababisha vile vile hali ya hatari kwa raia. Msaada unaotakiwa kwa sasa hivi, aliongeza kusema Holmes, utatumiwa kuwahudumia kihali raia waliongolewa makazi na wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) Ijumatano imetoa ‘Ripoti ya Uchunguzi wa Suala la Afyuni/Kasumba katika Afghanistan kwa 2009' ambayo ilibainisha biashara ya madawa haya ya kulevya imeanza kuonyesha dalili ya kupungua kwa mwaka huu. Takwimu zinaonyesha ukulima wa kasumba umeporomoka kwa asilimia 22, uzalishaji wa madawa ya kulevya umeanguka kwa asilimia 10, na wakati huo huo bei za madawa zimeshuka kwa kima ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa muda wa miaka kumi. Kadhalika, ripoti inasema idadi ya majimbo yaliofanikiwa kukomesha ukulima wa mazao ya kasumba imeongezeka kutoka asilimia 18 na kufikia asilimia 20 kwa hivi sasa, wakati idadi kubwa ya wachuuzi wa bidhaa haramu hizi inaendelea kukamatwa, kwa sababu ya operesheni kali na za nguvu za vikosi vya NATO pamoja na majeshi ya Afghanistan. Lakini Mkurugenzi Mkuu wa UNODC, Antonio Maria Costa alihadharisha vile vile kwamba uchunguzi wao umegundua makundi ya wahalifu yameonekana kuungana na wapinzani wa serikali wa Taliban kukwepa kukamatwa na kujipatia hifadhi ya kuendesha vyema biashara ya kasumba nchini mwao.

Naibu Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, Peter Galbraith ameripotiwa akieleza kwamba shambulio la bomu la kujitolea mhanga liliotukia kwenye msikiti wa Jimbo la Laghman, Afghanistan hii leo ni kitendo "kisioweza kutetewa abadan". Shambulio hili liliripotiwa kumwua naibu mkuu wa idara ya upelelezi ya Afghanistan, na vile vile kuua na kujeruhi maofisa kadha wa Serikali pamoja na raia wingi. Galbraith alishtumu kitendo hiki katili kinakwenda kinyume kabisa na matakwa ya umma wa Afghanistan, kwa ujumla, umma ambao, alitilia mkazo, una hamu kubwa ya kurudisha tena amani na utulivu kwenye taifa lao hasa katika mwezi mtukukufu wa Ramadhan.