Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon leo alizuru Mzingo wa Barafu wa Ncha ya Dunia (Polar Ice Rim) wakati alipokuwa ndani ya meli ya Norway. Kabla ya hapo KM na mkewe walizuru Steshini ya Zeppelin, kituo cha Norway kiliopo Kaskazini ya dunia, kunapoendelezwa uchunguzi wa hewa ya eneo la Akitiki, utafiti ambao hufuatilia athari za hewa chafu inayomwagwa angani pamoja na vichafuzi vyengine. KM alipata fursa ya kujionea binafsi majabali ya barafu yalionywea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hali ambayo alisema ilimshtusha sana. Ilivyokuwa chini ya siku 100 zimesalia kabla ya kufanyika Mkutano Mkuu wa Copenhagen juu ya Udhibiti wa Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa, KM alisema safari yake ya kaskazini ya ncha ya dunia imempatia fursa ya kujionea mwenyewe athari za mazingira, hali itakayomsaidia kuwahamasisha wajumbe watakaohudhuria Mkutano wa Copenhagen juu ya dharura ya kukamilisha mapatano ya mkataba mpya wa kuhifadhi mazingira, na kudhibiti bora athari chafuzi zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti ya kuwa mnamo mwisho wa wiki iliopita, watu 16 walizama katika Ghuba ya Aden kwa sababu ya matukio mawili yanayohusu safari za magendo zilizoanzia Usomali. Mapema Ijumamosi usiku mashua iliochukua watu 44 ilipinduka baada ya wafanya magendo kuwasukuma majini abiria, kwenye eneo la nje ya mwambao wa Yemen. Watu 34 kati ya abiria hawo waliweza kufika nchi kavu, na maiti saba zilipatikana na kuzikwa katika sehemu za ardhi jirani na shirika la kienyeji linalofanya kazi na UNHCR. Kwenye tukio la pili, inaaminika wafanya magendo, wakiogopa kukamatwa na wenye madaraka Yemen, waliwalazimisha abiria 42 kuogolea na kuelekea nchi kavu kutoka kwenye mashua waliokuwemo, karibu na mwambao wa Yemen. Taarifa ya UNHCR inasema watu 30 walifaulu kufika nchi kavu, na watu waliosalia waliripotiwa kuzama. UNHCR inasema katika siku tano zilizopita mashua 17, zilizokuwa zimechukua watu 835, ziliwasili Yemen baada ya kufanya safari hatari ya kuvuka Ghuba ya Aden kutokea eneo la Pembe ya Afrika.