Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yahadharisha, mzozo mkuu wa kiutu wajiandaa kuripuka Yemen kaskazini

UNHCR yahadharisha, mzozo mkuu wa kiutu wajiandaa kuripuka Yemen kaskazini

UM unaashiria mzozo mkubwa wa kiutu unajiandaa kufumka katika mji wa Sa\'ada, uliopo Yemen kaskazini, ambapo hali huko inaripotiwa kila siku kuendelea kuporomoka na kuharibika.

UM unakhofia usalama wa raia walionaswa ndani ya mji, kutokana na mapigano makali baina ya vikosi vya wapinzani wa Al Houthi na wanajeshi wa serikali. Mapigano haya sasa yameingia wiki ya tatu, kwa mujibu wa taarifa za Andrej Mahecic, msemaji wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR). Alisema watu 35,000 wamelazimika kuhama makazi yao katika Sa'ada na kwenye vitongoji vyake. Tangu 2004 wahamiaji wa ndani ya nchi 150,000 waliathirika na mapigano katika sehemu hiyo ya Yemen. Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mkuu wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) Ijumatano ataanzisha mjini Geneva kampeni maalumu ya kuomba UM ufadhiliwe misaada ya dharura, kuisaidia Yemen kukabiliana na mzozo wa Sa'ada. Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), kwa upande wake, linasema watu 100,000 waliokosa matumaini wanaendelea kuhama kwa kasi kutoka mji wa Sa'ada kutafuta hifadhi, kwenye maeneo yalio salama ya katika Jimbo la Sa'ada. WFP inakadiria idadi hiyo itaongezeka na kusababisha wahamiaji wa ndani (IDPs) ziada watakaofikia 150,000. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti asilimia kubwa ya miradi ya afya ya jamii, imesitishwa kwenye eneo la vurugu na vituo vyingi vya afya, ama vimefungwa au haviwezi tena kufikiwa na wahudumia afya au wagonjwa katika Sa'ada. Hali hii inakhofiwa huenda ikazusha maradhi hatari ya kuambukiza mbalimbali, kama shurua, malaria na ugonjwa wa kuharisha dhidi ya umma.