Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umma wa Dungu watishwa kila siku na mashambulio ya LRA, anasema Mkuu wa UNICEF

Umma wa Dungu watishwa kila siku na mashambulio ya LRA, anasema Mkuu wa UNICEF

Ann Veneman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) kwenye siku ya mwisho ya ziara ya siku tano alioendeleza katika JKK alipata fursa ya kukutana na wale watoto waliotoroshwa na waasi wa Uganda wa kundi la LRA.

Mkutano wao ulifanyika kwenye mji wa Dungu, eneo la mbali katika kaskakzini-mashariki ya JKK ambapo UM unakadiria tangu mwezi Disemba 2007 raia 320,000 waling'olewa makazi kwa sababu ya mashambulio na vurugu liliopamba kwenye eneo hilo. Waasi wa LRA ndio wanaotuhumiwa kuhusika na vifo 1,200 vya raia vilivyotukia mwezi Julai pekee katika mwaka huu. Veneman alisema "Wafuasi wa kundi la LRA wana sifa mbaya ya kuwatorosha watoto wa umri mdogo, na kuwalazimisha kuua na kuwalemaza waathirika wasio hatia, na papo hapo kuwageuza watoto wa kike mateka kama vimada wao." Kwa mujibu wa Veneman umma wa Dunga kila siku wanaishi na khofu ya kushambuliwa na waasi wa LRA, ambao kwa "muda wa miaka 20 walipalilia khofu na utawala wa vitisho katika baadhi ya sehemu za Uganda na katika nchi jirani." Alisema alishtushwa sana na miripuko ya vurugu pamoja na matumizi ya nguvu dhidi ya watoto katika JKK. Lakini alisema aliingiwa moyo sana kuona namna jamii ya Dungu inavyoonyesha "bidii na shauku ya kuwatazama watoto waliowakimbia waasi wa LRA, na kuwasaidia, kwa kila njia, watoto hawa kumudu maisha ya kikawaida."