Hapa na pale

Hapa na pale

Tarehe 31 Agosti ni siku ya mwisho ya uraisi wa duru wa Baraza la Usalama kwa Uingereza. Kuanzia tarehe mosi Septemba uraisi wa Baraza la Usalama utakabidhiwa Marekani. Ijumatano Balozi Susan Rice wa Marekani anatarajiwa kutangaza mradi wa kazi na ajenda ya Baraza la Usalama kwa mwezi Septemba.

Ijumatatu asubuhi KM Ban Ki-moon alikutana mjini Oslo na Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Mambo wa Nje wa Norway na walisailia natija za kuimarisha uhusiano wa kimataifa unaoshirikisha pande nyingi pamoja na kuzingatia majukumu ya Norway kwenye jumuiya ya kimataifa. Baada ya hapo, Waziri Mkuu wa Norway Jens Stoltenberg na KM walikutana na waandishi habari ambapo Ban Ki-moon alisema taifa la Norway ni miongoni mwa yale mataifa yenye "imani thabiti kuhusu maadili na malengo ya UM". Vile vile KM aliingiwa moyo sana na mchango mkubwa wa Norway katika shughuli za UM. Waziri Mkuu wa Norway aliahidi kwamba taifalao litafanikiwa kufadhilia asilimia 1.1 ya Jumla ya Pato la Taifa kuhudumia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa nchi maskini.

Makamu Mkuu mpya wa Jeshi la Wanamaji, Jürgen Mannhardt wa Ujerumani leo amekabidhiwa madaraka ya Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Vikosi vya Muda vya UM kwa Lebanon (UNIFIL) na atamrithi madaraka hayo Makamu Mkuu Ruggiero Di Biase wa Utaliana aliyemaliza muda wake wa kazi hivi karibuni. Kamanda Mkuu wa Vikosi vya UNIFIL, Meja-Jenerali Claudio Graziano alielezea kuwepo uhusiano wa kutia moyo kwa sasa hivi baina ya Jeshi la Wanamaji la UNIFIL na Jeshi la Majini la Lebanon, uhusiano ambao ulijengeka kutoka mazoezi ya mara kwa mara kwenye zile operesheni za kuzuia vitendo haramu visizuke kwenye eneo wanaolishughulikia. Kauli ya Meja-Jenerali Graziano ilitolewa wakati wa taadhima za upokezanaji wa madaraka ya Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la UNIFIL. Kwa mujibu wa UNIFIL tangu operesheni za wanamaji zilipoanzishwa katika tarehe 15 Oktoba 2006 Vikosi Maalumu vya Wanamaji wa UNIFIL vilifanya ukaguzi wa meli 27,000 na katika ya jumla hiyo meli 370 ziada zilipelekewa mamlaka halali katika Lebanon kuendeleza uchunguzi zaidi kuhakikisha meli hizo hazijabeba bidhaa zilizopigwa marufuku.

Wajumbe wa Serikali wanachama walikutana Ijumatatu kwenye Makao Makuu ya UM kujadilia usimamizi bora wa mazingira ya baharini. Taarifa ya Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) inasema licha ya majukumu makubwa yanayoendelezwa na bahari kuu, kumeonekena kuwepo pengo kubwa katika ufahamivu wa wanadamu kuhusu harakati na mazingira ya bahari, kwa ujumla. Ripoti ilisema pindi Serikali zitaweza kufikia makubaliano kwenye majadiliano yao ya sasa hivi, kuna uwezekano wa kuwa na makadirio kamili ya, awali, kimataifa, yatayounganisha taarifa za bahari zote za ulimwengu, itakapofika 2014. Naibu KM Asha-Rose Migiro alihudhuria mkusanyiko huo wa katika Makao Makuu ya UM, na kwenye taarifa alioiwasilisha mkutanoni aliwahimiza wajumbe wa kimataifa kuchukua hatua zitakazosaidia kuhakikisha tathmini hii mpya inatekelezwa kipamoja, kwa lengo la kuupatia umma wa kimataifa taarifa za jumla za mapitio ya matatizo yanayokabili mazingira ya baharini.