Siku 100 zimesalia kabla ya Mkutano wa COP-15 kudhibiti taathira za mabadiliko ya hali ya hewa

28 Agosti 2009

UM umetoa mwito maalumu wenye kuwataka mamilioni ya umma wa kimataifa kutia sahihi zao, kwenye mtandao, ili kuidhinisha lile ombi la kuzihimiza serikali wanachama Kukamilisha Makubaliano juu ya waraka wa Mkutano wa COP-15, yaani ule Mkutano Mkuu utakaofanyika mwezi Disemba katika mji wa Copenhagen, Denmark kuzingatia mkataba mpya wa udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

UM umetayarisha kampeni ya Wiki ya Udhibiti wa Mabadiliko ya Hewa, wiki ambayo itaadhimishwa kimataifa kuanzia tarehe 21 mpaka 25 Septemba mwaka huu, na itatumiwa kuhamasisha viongozi wa Nchi Wanachama kufikia muafaka wenye wizani, ulio wa haki na wenye wizani utakaoridhisha wote katika kudhibiti bora taathira haribifu za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Hivi sasa tumebakiza siku 100 kabla ya mkusanyiko wa Copenhagen, alisema KM Ban Ki-moon kwenye risala alioitoa wiki hii, ambapo pia alisistiza kwamba "muda hatunao tena, maana wataalamu wanahadharisha athari haribifu za mabadiliko ya hali ya hewa zimeonekana kuongeza kasi." Alisema kunahitajika uongozi wa kisiasa wa hali ya juu utakaohakikisha umma na dunia yetu huwa unapatiwa hifadhi inayofaa, na kuweka kichocheo kitakachokuza maendeleo ya mazingira ya kijani yenye natija kwa umma wotewa kimataifa katika karne ya 21.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud