Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanasheria wa Afrika Kusini ameteuliwa kutetea haki za wanawake waathirika wa matumizi ya nguvu

Mwanasheria wa Afrika Kusini ameteuliwa kutetea haki za wanawake waathirika wa matumizi ya nguvu

Taarifa iliotolewa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) imeleza kwamba wakili kutoka Afrika Kusini, Rashida Manjoo, ameanza rasmi kazi ya Mkariri (Mtetezi) Maalumu mpya wa UM atakayehusika na huduma za kupinga matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake, na kuendeleza kampeni za kudhibiti sababu na taathira za udhalilishaji wa kijinsiya.

Rashida Manjoo ni mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Afrika Kusini na kwenye kikao cha 11 cha Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu, katika mwezi Juni 2009, aliteuliwa kuwa Mkariri Maalumu dhidi ya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsiya, kwa kipindi cha mwanzo cha miaka mitatu. Bi Rashida alinakiliwa akisema "matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake ni kitendo kunachoharamisha hadhi ya utu pamoja na haki kadha za kimsingi, ikijumlisha usawa wa haki, ukamilifu wa mwili, uhuru wa maadili na haki ya mwanadamu kutobaguliwa." Alikumbusha ya kuwa "misingi ya kanuni za usawa na hifadhi kwa wanadamu inasisitiza juu ya wajibu kwa walimwengu kukabiliana, kikamilifu, na masuala yote yanayohusu matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake, na kutambua kwamba kitendo hiki kinaambatana na ubaguzi wa hali ya juu dhidi ya wanawake na kinakwenda kinyume na kanuni za kimataifa." Alisema hiyo ndio misingi itakayomwongoza yeye kwenye kazi zake. Mtaalamu huyu huru wa UM juu ya haki za binadamu ameshaendeleza tafiti kadha wa kadha juu ya suala la la haki za kijinsiya na vile vile alifundisha katika vyuo mbalimbali katika Marekani na Afrika Kusini, halkadhalika. Karibuni Rashida Manjoo alikuwa Profesa Mgeni katika Chuo Kikuu cha Webster, Marekani ambapo alikuwa akifundisha masomo juu ya haki za binadamu, na kulenga zaidi kwenye haki za wanawake na mfumo wa sheria ya mpito.