Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Asubuhi Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio la kuidhinisha operesheni za Vikosi vya UM vya Uangalizi wa Kusitisha Mapigano Lebanon (UNIFIL) ziendelee kwa miezi 12 zaidi katika eneo husika. Baada ya hapo wajumbe wa Baraza walisikiliza taarifa ya fafanuzi kutoka Jun Yamazaki, Mdhibiti Fedha wa UM, juu ya ripoti ya KM kuhusu Mfuko wa Maendeleo kwa Iraq. Kufuatia mashauriano hayo, kwenye taarifa iliotolewa kwa waandishi habari baadaye, wajumbe wa Baraza walibainisha kuingiwa wasiwasi kuhusu namna fedha za Iraq zinavyosimamiwa, na walisema wangelipendelea kuona marekibisho yanafanyika, haraka, kwenye utaratibu huo ili kuhakikisha Serikali ya Iraq inapewa madaraka zaidi kwenye matumizi ya rasilmali yao kutoka Mfuko wa Maendeleo.

Ijumatano, Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Agosti, Balozi John Sawers wa Uingereza alitangaza kwa waandishi habari, kwa niaba ya wajumbe wa Baraza, taarifa iliolaani, kwa kauli kali, lile shambulio la kigaidi liliotukia Ijumanne kwenye mji wa Kandahar, Afghanistan. Wajumbe wa Baraza la Usalama walitilia mkazo kwenye taarifa yao ya kuwa wanataka kuona watu waliosababisha jinai hii wanashikwa haraka na kufikishwa mahakamani kukabili haki.

Martin Mogwanja, Mratibu wa UM juu ya Misaada ya Kiutu kwa Pakistan karibuni alifanyisha kikao cha maofisa wanaowakilisha mashirika ya UM ambao walitathminia hali katika Wilaya ya Swat, eneo lilioshuhudia mapigano makali katika miezi michache iliopita. Kadhalika, Mogwanja alipata fursa ya kukutana na wawakilishi wanaoendesha serikali za wilaya na wajumbe wa mashirika yasio ya kiserikali ya kitaifa na kimataifa yaliopo Pakistan, ambao wote walikubaliana kwamba kazi za kufufua shughuli za kiuchumi na jamii katika Wilaya ya Swat ni lazima zianzishwe haraka. Kwa mujibu wa tathmini yao miundombinu ya sekta ya raia pamoja na viambajengo vya umma vimeonekana vinafanya kazi, lakini vimechakaa na vibovu, na vinahitajia marekibisho ya hali ya juu, mathalan vifaa vya mawasiliano, vinu vya umeme, mitandao ya kugawa maji, majengo ya skuli na pia yale majengo ya kuhudumia afya yote yanahitajia marekibisho. Kwa mujibu wa Dktr. Eric Laroche, Katibu Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watu milioni 1.5 wamesharejea makwao ambapo walikuhama wakati wa mapigano. Lakini alisikitika kwamba majengo ya afya na mali za watu kwenye wilaya yaliharibiwa, kuibiwa na kuangamizwa. Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti Wilaya ya Swat vile vile itahitajia misaada ya dharura ya chakula kwa sababu wakazi wa eneo hilo walipoteza asilimia 85 ya akiba ya mazao ya mavuno yaliopita.

Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na mashirika wenzi wametayarisha vielekezi vipya kuhusu mafunzo ya ujinsia. Lengo la mwongozo huu ni kuwapatia walimu zana za kuwailimisha watoto kuhusu namna ya kujikinga na mateso ya unyanyasaji, uonevu na kujamiiwa kimabavu. Kadhalika miongozo hii hujumuisha mafunzo kinga dhidi ya mimba isiokusudiwa, na kuwapatia hifadhi ya maambukizi ya maradhi yanayotokana na kujamiana, ikiwemo UKIMWI. Kwa mujibu wa taarifa za UNESCO maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanaweza kupunguzwa miongoni wa vijana pindi fungu hili la umma litapatiwa mafunzo yanayofaa, ilimu ambayo hukosekana katika sehemu nyingi za dunia. Takwimu za Jumuiya ya Mashirika ya UM Kupiga Vita UKIMWI (UNAIDS) pamoja Shirika la Afya Duniani (WHO) zimeonyesha vijana milioni tano ziada wanaishi sasa hivi katika dunia na virusi vya UKIMWI, na asilimia 45 ya maambukizi yote mapya ya maradhi haya hukutikana miongoni mwa vijana kati ya umri wa miaka 15 mpaka 24.