Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM alishtushwa na alishangazwa, halkadhalika, kuhusu shambulio liliotukia Ijumanne usiku kwenye mji wa Kandahar, Afghanistan ambapo ilripotiwa raia zaidi ya arobaini waliuawa na tukio hilo na raia themanini wengine walijeruhiwa. KM alishtumu,kwa kauli kali, kitendo katili hiki kisofahamika. KM aliwatumia aila zote za waathirika mkono wa pole, na vile vile aliwaombea majeruhi kupona haraka.

Kwa mujibu wa msemaji wa UM, KM ametoa shukrani zake za dhati kwa mchango wa Rodolpho Adada, Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur (UNAMID) aliyeongoza shughuli za shirika hilo katika miaka miwili iliopita, kwa ubora wa aina ya pekee. Adada atakamilisha muda wa kazi na UNAMID katika mwisho wa Agosti 2009. Mjumbe Maalumu huyu wa UNAMID ndiye aliyesaidia kuanzisha shirika la mchanganyiko la kurudisha amani Darfur, na kuliongoza kikazi katika kipindi kigumu kabisa pale vikosi vya polisi na wanajeshi vilipoenezwa, kwa mara ya kwanza, kwenye maeneo ya Jimbo la Magharibi la Sudan la Darfur.

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limetoa taarifa yenye masikitiko, na iliolaani vikali mauaji ya mwandishi habari yaliotukia mnamo usiku wa 22 Agosti 2009, kwenye mji wa Bukavu, Kivu Kusini. Mwanahabari huyu, anayeitwa Bruno Koko Chirambiza, alikuwa akifanya kazi na steshini huru moja ya redio. MONUC imewaomba maofisa wanaoshughulikia utawala wa sheria, kuwasaka wale walioendeleza jinai hii na kuwafikisha mahakamani, kitendo ambacho kikikamilishwa, inaaminika huenda kikasaidia kukomesha mauaji ya waandishi habari yanayofanywa kihorera na watu wasiojali adhabu.

Imeripotiwa na Shirika la UM juu ya Amani katika Liberia (UNMIL) ya kwamba mmoja wa watumishi raia wa kimataifa, kutoka Marekani, aliokuwa akichunguzwa kwa madai ya kushiriki kwenye ukandamizaji wa kijinsiya na kunajisi mtoto wa umri mdogo kimahakama, alikutikana amefariki kwenye makazi yake mjini Monrovia mnamo tarehe 24 Agosti. Chanzo cha kifo hakijulikani kwa sasa na kinafanyiwa uchunguzi na UNMIL. Kadhalika upelelezi kamili unaendelea juu ya madai dhidi ya mtumishi huyo wa UNMIL ya kunajisi mtoto mdogo na makosa mengine ya kijinsiya.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati amelikaribisha tangazo la WaFalastina wenye mamlaka juu ya ujenzi wa taifa. Alisema UM utaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Falastina kwenye ujenzi wa maeneo yao. Alisema kwamba mradi mpya wa WaFalastina ulioandaliwa kujenga taifa ukitekelezwa utawahamasisha makundi yote yanayohusika na hali ya Mashariki ya Kati, kupiga hatua, na kusonga mbele kwa mafanikio, kulitatua suala hili katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Kwa kuambatana na kiashirio hicho, aliongeza kusema, kutahitajika kupata ushirikiano wa Israel, pamoja na kupokea msaada maridhawa wa fedha kutoka wahisani wa kimataifa.