Msaada wa dola 500,000 wafadhiliwa na UNICEF kuhudumia miradi ya kijamii Kongo-Brazzaville
Ann Veneman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) ametangaza wakati anazuru Jamhuri ya Kongo (Brazzavile) wiki hii ya kuwa watafadhilia msaada wa dola 500,000 ili kuhudumia miradi ya lishe bora, afya na ilimu nchini humo, sekta ambazo ziliathiriwa zaidi na mizozo ya uchumi wa dunia na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wale raia walio dhaifu kihali.
Veneman alisema wanawake na watoto ndio fungu la raia lenye kuathirika sana na matatizo ya umaskini. Taarifa ya UNICEF ilisema Jamhuri ya Kongo inajitahidi, kwa sasa, kufufua shughuli za uchumi na jamii baada ya kumalizika vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, hali ambayo ilisababisha watu milioni 1 kung'olewa makazi. UNICEF iliongeza kusema kwamba baada ya mapatano ya amani kutiwa sahihi katika 2003, na yale makundi yaliohusika na mapigano, ilibainika kwamba zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini humo huwa wanaishi maisha duni, chini ya kiwango rasmi cha umaskini. Veneman alikumbusha vile vile kwenye taarifa yake ya kuwa katika kila watoto wanane wanaozaliwa ndani ya Jamhuri ya Kongo, mtoto mmoja kati ya hawo hufariki kabla hajatimia umri wa miaka mitano, kwa sababu ya maradhi yanayoweza kuzuilika.