Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imeomba dola milion 230 kuhudumia dharura ya chakula Kenya

WFP imeomba dola milion 230 kuhudumia dharura ya chakula Kenya

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) leo limetoa ombi la kutaka lifadhiliwe na wahisani wa kimataifa, msaada wa dola milioni 230 kuhudumia dharura ya chakula kwa Kenya katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Msaada huu utawapatia chakula watu milioni 3.8 walioathirika na hali mbaya sana ya ukame iliotanda nchini katika kipindi cha karibuni, hali ambayo imekuwa ngumu zaidi kwa watu wa kawaida kutokana na bei ya juu ya chakula. Kwa mujibu wa taarifa ya WFP sehemu nyingi za nchi zilinyimwa zile mvua za muda mrefu, za kila mwaka, ambapo katika majira manne yaliopita hakujanyesha mvua. Kadhalika, mavuno ya mahindi katika Kenya yanaashiriwa kupungua kwa asilimia 28, chini ya kiwango cha wastani. WFP inasema bei ya chakula inaendelea kupanda nchini Kenya, na wakati huo huo bei ya mifugo imeonekana kuteremka kwa kasi kabisa, kwa sababu ya kufifia kwa maeneo ya malisho ya wanyama na kupungua kwa akiba ya maji. Hivi sasa Shirika la WFP linajitayarisha kupanua zaidi zile operesheni za kuwapatia watoto wa skuli ziada 100,000 chakula, kadhia ambayo itajumlisha watoto wa skuli watakaofadhiliwa msaada huo kwenye yale maeneo ya Kenya yalioathirika na ukame sawa na karibu milioni 1.2.