Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa Juu ya Jinai ya Halaiki (ICC), yaani Luis Moreno-Ocampo Ijumatatu aliwakilisha hoja zake kwa Mahakama Ndogo ya Rufaa ya kupendekeza mtuhumiwa Jean-Pierre Bemba wa JKK, abakie kifungoni mpaka mwisho wa kesi. Vile vile alitaka Bemba asiachiwe wakati ombi la Mwendesha Mashitaka linazingatiwa na Mahakama ya Rufaa. Bemba alituhumiwa kushiriki kwenye makosa ya jinai yaliofanyika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

 Ahmedou Ould-Abdallah, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali alituma salamu muhimu mnamo mwanzo wa mwezi mtukufu wa WaIslam wa Ramadhan, inayowataka Wasomali wote kuongeza bidii za pamoja zinazotakikana kuwasilisha amani na utulivu hakika wa taifa lao katika kipindi hiki. Alinakiliwa akisisitiza kwenye risala hiyo ya kwamba "mazungumzo ya kuleta amani ni bora kwao badala ya mikwaruzano yauhasama ambapo Wasomali huwa wanaua Wasomali wenziwao."

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti mapigano yaliofura siku za karibuni, baina ya waasi wa Al Houthi na vikosi vya serikali katika Yemeni ya kaskazini, yameharibu zaidi yale mazingira magumu ya kihali yaliotanda kwenye maeneo ya uhasama. UNHCR inasema imeingiwa wasiwasi hasa na kuharibika kwa utulivu kwenye eneo la Sa'ada, mji mkuu wa Jimbo la Sa'ada, ambapo tangu tarehe 10 Agosti 2009 wakazi wa huko walinyimwa maji na umeme, na kwa sababu ya ukosefu wa usalama walishindwa hata kwenda marikiti kununua vyakula. Kadhalika katika jimbo jirani la Hajjah, kusini-magharibi ya Sa'ada, UNHCR inaendelea kusajili wale raia wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) na inaendeleza operesheni za kugawa mahema, maturubali ya plastiki, mablanketi na majerikeni ya maji. Shirika la Hilali Nyekundu la Yemen, likisaidiwa na UNHCR pamoja na wenye madaraka wa serikali za kienyeji katika Hajjah, wamejumuika kutengeneza kambi mpya ya kuwapokea waahamiaji. Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) inasema wahudumia misaada ya kiutu, kwa hivi sasa, wameshindwa kuwafikia wale waathirika wa mapigano kutathminia mahitaji yao kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Ijumanne kwenye mji wa El Fasher, kundi la kwanza la vikosi vya polisi maalumu 100 wa FPU, kutoka Jordan waliwasili kujiunga na Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID). Kundi la pili la maofisa wa polisi wa Jordan 180 wanatazamiwa kuwasili Ijumatano. Polisi hawa watatawanywa kwenye mji wa El Fasher na katika mji wa Kabkabiya uliopo Darfur Kaskazini. Kwa mujibu wa taarifa za UNAMID, kikawaida Washauri wa Polisi NA Unamid huwa ni maofisa wa polisi wasiochukua silaha, wenye jukumu la kufanya doria, kuchunguza matukio fulani na kutayarisha ripoti, pamoja na kusimamia ulinzi wa wahamiaji wa katika ndani ya nchi (IDPs). Ama polisi wa UNAMID wa FPU wenziwao, kwa upande mwengine, huwa ni aina ya polisi wa kikosi kimoja, wanaojitegemea, na wenye ujuzi maalumu na uwezo wa kuitika haraka, pakizuka mazingira ya hatari, na kudhibiti hali ya wasiwasi mapema zaidi. Polisi wa FPU vile vile wanao uzoefu wa kudhibiti makundi makubwa ya watu na operesheni nyengine za polisi zinazoambatana na usalama wa raia. Maofisa maalumu wa polisi wa FPU kutoka Jordan ni kundi la tano kuenezwa Darfur, kufuatia polisi wa namna hiyo kutoka Bangladesh, Indonesia, Nepal na Nigeria.

Rodolphe Adada, Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) Ijumatatu alizuru mji wa Nyala, Darfur Kusini na alikutana na watumishi wa UNAMID pamoja na wafanyakazi wakazi wa UM katika Sudan. Alifanya ziara ya hishima kwa Naibu Wali (Gavana) wa Darfur Kusini, Dktr Farah Mustapha. Ijumanne Adada pia alizuru El Geneina na Zalingei, miji ya Darfur Magharibi na kukutana na wakuu wa maeneo hayo, ikiwa ziara za mwisho kikazi za Adada kabla hajakamilisha muda wake kama Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UNAMID mnamo tarehe 31 Agosti 2009.

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ametoa taarifa yenye kukaribisha uamuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Marekani wa kumteua mwendesha mashitaka maalumu wa kuchunguza kama maofisa wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), pamoja na wakandarasi wa usalama, walikiuka sheria za Marekani pale walipowasaili na kuwadadisi, kwa kutesa, wale watu waliowaweka vizuizini nje ya Marekani, ikijumlisha wafungwa waliowekwa vizuizini katika Guantanamo Bay, Cuba. Pillay alisisitiza vitendo vya kutesa watu bila kukhofu adhabu, au kuwatendea watu walio kizuizini mambo yaliokwenda kinyume na sheria katika Marekani na katika sehemu nyengine za dunia ni lazima yahukumiwe na sheria. Aliongeza kwa kusema mtindo wa kutumia maeneo ya siri kuwaweka watu vizuizini ukomeshwe, na alitoa mwito unaotaka majina ya watu waliowekwa kwenye vituo hivi vya siri yatangazwe rasmi hadharani. Pillay aliunga mkono ahadi ya Raisi wa Marekani ya kuifunga ile kambi ya wafungwa ya Guantanamo itakapofika 2010, na kumtaka afanye mapitio, ya dharura, kuhusu hali ya wafungwa waliowekwa kizuizini katika viambajengo vya Bagram, Afghanistan. Kadhalika Pillay alikaribisha uamuzi wa kumwachia huru kutoka kambi ya kizuizi ya Guantanamo Bay, raia mmoja wa Afghanistan ambaye alipokamatwa mnamo miaka ya nyuma na kutiwa ndani na vikosi vya Marekani kwenye kambi hiyo, alikuwa na umri wa miaka 12.