Mhudumia misaada ya kiutu wa kimataifa awapatia sauti wanusurika wa madhila ya kijinsiya katika JKK

21 Agosti 2009

Ijumatano ya tarehe 19 Agosti (2009) iliadhimishwa na UM, kwa mara ya kwanza katika historia yake, kuwa ni ‘Siku ya Kumbukumbu kwa Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani.\'

Kwa muda wa miaka miwili na nusu, Roselidah Ondeko, aliitumikia UNFPA kwenye eneo la mashariki la JKK, akiwasaidia wanawake wenyeji kujipatia sauti ya kujitetea hadharani dhidi ya mateso yanayoambatana na janga la udhalilishaji wa kijinsiya, ikichanganyika na matumizi ya mabavu ya kutesa wanawake. Roselidah ni mratibu wa mradi maalumu wa kudhibiti matatizo yanayohusiana na udhalilishaji wa kijinsiya katika majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, mradi ambao ulifadhiliwa msaada wa fedha na Shirika la Kanada juu ya Maendeleo ya Kimataifa (CIDA). Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) eneo la mashariki la JKK ni sehemu ambayo mapigano hushtadi mara kwa mara baina ya waasi na vikosi vya serikali, na ni eneo ambalo pia limesajiliwa kufanyika, kwa wingi kabisa makosa ya kunajisi kimabavu raia, hususan wanawake.

Roselidah alisema mara ya kwanza alipojaribu kusikiliza ripoti za mateso waliopitia wanawake wa eneo hili alipata shida sana. Kwa hivyo, kwa yeye kuweza kuzisikiliza tena ripoti zinazohusu mateso kama hayo ya kijinisya, kwa makini zaidi, kutoka wanawake waliokuwa wakihitajia matibabu ya mwili na kiakili, Roselidah alilazimika kumwomba mfanyakazi mwengine mwenye ujuzi kama wake kumshindikiza na kuwa naye kwenye vikao hivyo. Alikumbusha kwamba waathirika wanawake wa unyanyasaji wa kijinsiya katika JKK ni watu waliovumilia maumivu ya kila aina, lakini wao pia ni watu walioonyesha ujasiri mkubwa kwa kukataa kabisa kushindwa kimaisha kwa sababu ya maafa hayo, na siku zote walibashiria matumaini ya kutia moyo kwa siku za usoni. Roselidah aliwaita fungu la wanawake hawa walioteswa kijinsiya ‘wanusurika' badala ya ‘waathirika'. Alitoa mfano wa mwanamke mmoja ‘mnusurika' ambaye katika 2007 alinajisiwa kimabavu katika Kivu, na baada ya mumewe kutambua kama mkewe alipatwa na maafa hayo, alimwacha bila ya msaada wa aina yoyote wa kumudu maisha. Lakini kutokana na mradi anaosimamia Roselidah wa UNFPA, mwanamke mnusurika alibahatika kupewa mbuzi mmoja wa kumsaidia kujipatia pato la kuendesha maisha. Kufuatia hapo, katika mwaka 2008 mwanamke huyo huyo aliweza kuwa na mbuzi sita badala ya yule mmoja aliyefadhiliwa na mradi wa UNFPA. Alihisi kwamba kulalamika peke yake juu ya maafa alioyapitia SIKU ZA NYUMA, hakutompeleka popote kimaisha, ndipo alipoamua kujitegemea, binafsi, ili aweze kuwahudumia maisha mema watoto wake.

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu (UNFPA) baina ya miezi ya Januari hadi Juni mwaka huu kesi zilizoripotiwa kutukia, kuhusu unyanyasaji na matumizi ya nguvu pamoja na udhalilishaji wa kijinsiya ziliongezeka tukilinganisha na kipindi hicho hicho katika mwaka jana. Roselidah alieleza kwamba wanawake wingi walihamasishwa kuripoti mateso hayo kwa sababu ya kurejea hali tulivu kwenye eneo lao na kwa sababu ya mchango wa mradi wa UNFPA, unaowahimiza wanawake kuwa na madaraka ya kujitegemea. Aliongeza kusema kwamba wanusurika wa makosa ya jinai ya kudhalilisha wanawake hivi sasa wanaweza pia kufikia matibabu ya madhila yao kwa urahisi, ambapo vile vile huwa wanahudumiwa tiba ya kudhibiti taathira za kiakili kutokana na maafa waliopitia, huduma ambazo siku za nyuma zilikuwa shida kupatikana kwa sababu ya ukosefu wa usalama katika eneo.

Taarifa za UM zinasema wakosaji wa vurugu la kijinsiya katika Majimbo ya Kivu wligunduliwa mara nyingi kuwa ni wale raia wenye kuvaa sare, yaani wapiganaji, wakijumuisha askari wa jeshi la JKK na wapiganaji waasi. Alisema Roselidah watoto waliopo maeneo ya Kivu nawo vile vile waliathirika na jinai ya kunajisiwa wanawake kimabavu. Alibainisha kwenye mahojianoaliokuwa nayo na Kituo cha Habari cha UM ya kwamba kabla ya yeye kupelekwa majimbo ya mashariki katika JKK kufanya kazi, alitumikia Shirka la UNFPA katika jimbo la magharibi la Sudan la Darfur na pia katika Uganda. Anasema akilinganisha hali ya wanusurika wa maafa hayo kati ya Kongo na Darfur, aliona wanawake wa JKK waliosaidiwa na mradi wa UNFPA, huwa na uwezo mkubwa wa kujieleza, binafsi, hadharani kuhusu madhila waliopata ya kunajisiwa kimabavu, madaraka ambayo yamewaponyoka wanawake wa Darfur.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter