WFP inasema hali ya chakula Darfur inatia wasiwasi

WFP inasema hali ya chakula Darfur inatia wasiwasi

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), ambalo linahudumia misaada ya kihali kwa watu milioni 3.6 katika Jimbo la Magharibi la Sudan la Darfur limeripoti kukabiliwa na majukumu ziada baada ya mashirika wenzi, yasio ya kiserikali, kufukuzwa Sudan mnamo mwanzo wa mwaka huu.

Ufukuzaji huo umewafanya wahisani wakuu wanne waliokuwa wakifadhilia huduma za WFP katika Darfur kuamua kusitisha michango yao, hali ambayo imezusha vizingiti kadha kwenye operesheni za ugawaji chakula kwa waathirika wa mgogoro wa Darfur. Imeripotiwa pia ya kuwa katika baadhi ya sehemu ya zile kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs), wanamoishi WaDarfuri milioni 2, mapigano ya hapa na pale yanayozuka huko, mara kwa mara, husababisha wakazi wa maeneo hayo kuhama tena kambi hizo na kuelekea sehemu nyengine za jimbo kutafuta hifadhi. Hali hii, kwa mujibu wa WFP, huwasilisha matatizo ziada kwenye shughuli zao za ugawaji wa chakula kwa wahamiaji muhitaji. Hata hivyo, WFP imeripoti akiba ya chakula, kwa ujumla, ni afadhali katika kipindi cha hivi sasa. WFP inaamini mzozo wa Darfur hautofanikiwa kuhitimishwa bila ya, kwanza, kupatikana maafikiano hakika ya kisiasa miongoni mwa yale makundi yanayohasimiana. Kadhalika WFP imeripoti itahitajia msaada wa dola milioni 870 katika mwaka ujao (2010) kuendeleza operesheni zake nchini Sudan. Halkadhalika ripoti ya WFP imeeleza kwamba sasa hivi inahudumia chakula vile vile wahamiaji milioni 1.6 ambao huishi kwenye vijiji vya mbali vya katika Darfur, na kuwapatia msaada huo pia wale wahamiaji wenye kuishi kwenye miji na jamaa zao.