UM inawakumbuka na kuhishimu wahudumia misaada ya kiutu duniani

UM inawakumbuka na kuhishimu wahudumia misaada ya kiutu duniani

Siku ya leo inaadhimishwa na UM, kwa mara ya kwanza kihistoria, kuwa ni ‘Siku ya Kumbukumbu kwa Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani.\'

 Baraza Kuu la UM mwaka jana lilipitisha azimio la kuitambua tarehe 19 Agosti, kila mwaka, kuwa ni siku ya kukumbuka juhudi za msitari wa mbele za watumishi wa UM wanaohudumia misaada ya kiutu na kihali katika sehemu mbalimbali za dunia. Tarehe hiyo iliidhinishwa na wajumbe wa kimataifa, kwa sababu inaambatana na ile tarehe ya 19 Agosti 2003, ambapo makao makuu ya ofisi za UM katika Hoteli ya Kanali, Baghdad yalihujumiwa na mabomu, na watumishi 22 wa UM waliuawa, akiwemo mjumbe wa hadhi ya juu wa UM, Sergio Vieira de Mello, na watu 150 wengine walijeruhiwa. Kunafanyika taadhima kadha wa kadha hapa Makao Makuu mnamo siku ya leo, na vile vile kwenye ofisi nyengine za UM, ambapo umma wa kimataifa hukumbushana juu ya mchango wa wahudumia misaada ya kiutu ulimwenguni, watumishi wa kimataifa ambao baadhi yao walipoteza maisha wakati wakijitahidi kutekeleza majukumu yao ya kuwaokoa watu waliokabiliwa na maafa, ili nawo wamudu maisha kama inavyotakikana. Kwenye risala ya KM alioiwasilisha leo asubuhi katika taadhima za Makao Makuu, juu ya ‘Siku ya Kumbukumbu kwa Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani' alisema taadhima hizi zimeksudiwa hasa kuhamaisha umma wa kimataifa, kutambua "mhanga wanaotoa wahudumia misaada ya kiutu kwenye kazi zao ... ambapo lengo lao hakika hasa ni kukidhi mahitaji ya mamilioni kwa mamilioni ya umma unaotegemea mchango huo kunusuru maisha." KM aliorodhesha aina ya watu wanaotegemea misaada ya kihali kutoka taasisi za UM - ikijumlisha "watu bilioni moja wanaosumbuliwa na njaa, makumi milioni ya umma uliolazimika kuhajiri makwao kwa sababu ya mapigano, mikwaruzano na maafa ya kimaumbile; na vile vile wale watoto wanaofariki kutokana na maradhi ambayo walimwengu wana uwezo wa kuyatibu; na pia watoto wa kike na wanawake wanaoteswa na kudhalilishwa kikatili kijinsiya." KM alitaka mizizi ya matatizo haya yashughulikiwe na kutokomezwa mapema. Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetoa takwimu zilizothibitisha katika mwaka 2008 wahudumia misaada ya kiutu 260 walishambuliwa, na kati yao idadi hiyo baadhi yao waliuawa, wengine walitekwa nyara na wenziwao kadha walijeruhiwa vibaya kabisa.