Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon ametoa taarifa maalumu inayowahimiza WaAfghani, wa kiume na kike wanaostahili kupiga kura, kushiriki kwenye uchaguzi ujao wa Uraisi na Baraza la Majimbo, utakaofanyika nchini tarehe 20 Agosti 2009. Alisema kushiriki kwao kwenye uchaguzi huo, utaisaidia Afghanistan kuimarisha zaidi taasisi za kidemokrasia nchini na kuongeza nguvu za mifumo ya kisiasa na, hatimaye, kuzikamilisha zile ahadi za kuchangisha ustawi na amani katika Afghanistan. Vile vile KM aliwasihi wagombea uchaguzi wote, pamoja na wafuasi wao, na mawakala wa vyama vya kisiasa, na pia waangalizi wa uchaguzi wa kizalendo na wa kimataifa, kuendelea kushirikiana na Kamisheni Huru ya Taifa Inayosimamia Uchaguzi pamoja na zile taasisi nyengine katika Afghanistan, na vile vile kushirikiana na wadau wa kimataifa wanaosaidia kwenye matayarisho ya uchaguzi, ili kuhakikisha mfumo wa kupiga kura utaendeshwa kwa mafanikio na bila ya shida.

Asubuhi Baraza la Usalama lilifanyisha mkutano juu ya Mashariki ya Kati. Oscar Fernandez-Taranco, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa alipohutubia wajumbe wa Baraza alieleza kwamba Kamati ya Muda ya Mawasiliano, ambayo huratibu misaada ya wahisani binafsi kwa umma wa Falastina, pamoja na wawakilishi wa Kundi la Wapatanishi wa Pande Nne juu ya Mashariki ya Kati wanatarajiwa kukutana Makao Makuu mwezi Septemba kwenye pambizo za kikao kijacho cha mwaka cha Baraza Kuu. Wanatarajiwa pia kushauriana na wawakilishi wa kamati ya kufuatilia ya Umoja wa Nchi za KiArabu kuhusu Pendekezo la Amani kwa Mashariki ya Kati la Mataifa ya KiArabu. Fernandez-Taranco aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba amezikaribisha hatua za karibuni za Israel za kupunguza vikwazo dhidi ya haki ya WaFalastina kutembea na kuzuru eneo liliokaliwa la Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan. Alisema mabadiliko yanayotakikana kuleta amani ya eneo hayatofanikiwa kukamilishwa bila ya kuchukuliwa hatua kama hizo muhimu. Hata hivyo alisema vitendo vya walowezi vya Israel katika eneo la Jerusalem Mashariki na kwenye Ufukwe wa Magharibi vimewasilisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya kimataifa kuhusu amani ya eneo la mvutano. Kadhalika Fernandez-Taranco alisema mashauriano yao na wenye madaraka Israel bado yanaendelea kuhusu pendekezo la UM liitakayo Israel kuruhusu kuanzishwa haraka shughuli za kuyatengeneza majengo yalioharibiwa na mashambulio ya mwanzo wa mwaka katika Tarafa ya Ghaza, hasa yale majengo ya maskuli, nyumba za makazi na zahanati za afya. Kuhusu Lebanon, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa Fernandez alieleza hali kijumla huko imesalia kuwa ni shwari, kwenye yale maeneo ya operesheni za Vikosi vya Muda vya UM katika Lebanon (UNIFIL). Lakini alisema ndege za vita za Israel bado zinaendelea kuruka kiharamu kwenye anga ya Lebanon takriban kila siku, kinyume na kanuni za kimataifa. Fernandez-Taranco alimaliza taarifa yake katika Baraza la Usalama kwa kuyasihi makundi husika yote kuwa na mwelekeo unaofaa, kwenye zile jitihadi zao za kubuni mazingira yatakayofufua haraka na kukamilisha kwa mafanikio, majadiliano ya amani baina ya Israel na WaFalastina ili kusukuma mbele maendeleo yatakayowasilisha amani ya jumla kieneo.

Choi Young-jin, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire ameripotiwa kuzuru maeneo ya ndani ya taifa hilo la Afrika Magharibi kutathminia miradi midogo-midogo ya shirika la UM la kulinda amani la UNOCI. Vile vile alipata fursa ya kuchunguza maendeleo katika ukusanyaji wa taarifa zinazoambatana na upigaji kura, ikijumlisha zile shughuli za usajili wa wapigaji kura pamoja na ugawaji wa vitambulisho. Ijumanne Choi alizuru mji wa Bouaké ambapo UM ulifadhilia misaada malumu kwa wapiganaji wa zamani wa kundi la Forces Nouvelles kuwasaidia kujiunga tena maisha ya kikawaida ya jamii, hususan wale vijana dhaifu na wanawake walioathirika na mapigano. Lengo la ziara za Mjumbe wa KM kwa Cote d'Ivoire kwenye maeneo ya bara ni kuhakikisha kunakuwepo mazingira ya utulivu na amani nchini, kabla ya uchaguzi kufanyika mwezi tarehe 29 Novemba 2009.