Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ijumanne amemaliza ziara yake katika Jamhuri ya Korea/Korea ya Kusini. Kabla ya kuondoka mji mkuu wa Seoul, KM alizuru madhabahu ya kuomboleza yaliopo hospitali, kumhishimu aliyekuwa Raisi wa Jamhuri ya Korea, Kim Dae-jung, ambaye alifariki siku ya leo.

Kutokana na mzozo uliofumka Yemen kaskazini hivi sasa, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa limetuma misaada ya vifaa vya kufanyia operesheni 200 kwa waathirika wa majeraha ya vihoro na viwewe vinaotokana na mazingira hayo. Kadhalika, WHO inajiandaa kupeleka Yemen wiki ijayo bidhaa zaidi ya vifaa na zana za matibabu. Hivi sasa wahudumia afya kadha kutoka ofisi ya kikanda ya WHO, iliopo Cairo, wameshaekwenda Yemen kusaidia shughuli za dharura za afya. Kadhalika WHO imejiunga na Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), kuratibu mpango wa dharura utakaosimamia huduma za afya na lishe bora.

UM Ijumatano ya tarehe 19 Agosti (2009) utaadhimisha kwa, mara ya kwanza, ‘Siku ya Kumbukumbu kwa Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani.' Kwenye mkesha wa siku hiyo, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay ametoa taarifa yenye kushtumu ya kuwa mauaji ya wafanyakazi wanaojitahidi kuwasaidia binadamu wenziwao kihali, ni jinai ya aibu na fedheha kuu kwa wanadamu, na ni kosa ambalo serikali zote zinawajibika kujiunga kulizuia - na pindi serikali zitashindwa kutoa kinga hiyo watuhumiwa wa makosa dhidi ya wahudumia misaada ya kiutu waadhibiwe. Alisema haki za binadamu zinafungamana kihakika pamoja na shughuli za kiutu, na alitilia mkazo kwamba mara nyingi ukiukaji wa haki za kibinadamu ndio kitendo cha awali kinachochea mizozo ya kiutu. Aliongeza, kwamba bila ya misaada ya kiutu, mamilioni ya umma wa kimataifa watanyimwa haki zao halali za kimsingi. Vile vile Kamishna Pillay alikumbusha ya kuwa tarehe 19 Agosti inaambatana na ile siku ya aibu ambapo mnamo mwaka 2003 kwenye Hoteli ya Canal, Baghadad, zilipokuwepo ofisi za UM katika Iraq, watu 22, wingi wao wakiwa watumishi wa UM waliuawa na shambulio la bomu. Alisema, kwa huzuni, kwamba tangu wakati huo wafanyakazi kadha wa UM na wa mashirika kadha mengine yasio ya kiserikali wenye kujitolea kuhudumia misaada ya kihali, walilengwa kwa mashambulio ya mabomu dhidi yao na kuuawa - na tukio lilioishtusha zaidi jumuiya ya kimataifa ni lile shambulio la tarehe 11 Disemba 2007 kwenye majengo ya UM ya Algiers, Algeria ambapo wafanyakazi 17 wa UM waliuawa.

Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwenye risala yake ya kuihishimu ‘Siku ya Kumbukumbu kwa Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani' alisihi umuhimu wa walimwengu kuwa thabiti na imara kwenye bidii za kuhudumia umma muhitaji, hasa katika mazingira ya ulimwengu uliokithiri hali za dharura kupita kiasi kwa sasa hivi, na aliutaka umma wa kimataifa kuwa wepesi kuitika maombi ya kusaidia kihali kwenye "sehemu zenye vurugu kuu la kisiasa" duniani. Aliahidi kwamba WHO ipo tayari kuitika maombi ya kitaifa na kimataifa kwenye utekelezaji wa mahitaji ya dharura ya afya.

Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) leo limetangaza matokeo ya tathmini kuhusu juhudi za mji wa Shanghai katika kuandaa maonyesho ya Expo-2010, yatakayotunza kwa urafiki mazingira ya hafla, kwa ujumla. Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa UNEP amesema kwenye taarifa hiyo ya UNEP kwamba maonyesho ya Shanghai Expo yameupatia ulimwengu fursa ya kushuhudia upenyu wa mazingira yaliotunzika bora kwa siku za baadaye. Alisema licha ya kuwepo vizingiti kadha wa kadha kwenye mazingira ya maonyesho, jiji la Shanghai limefanikiwa kukabiliana nayo kwa kuwasilisha mageuzi ya kisasa yatakayotumiwa kama ni mifano imara ya utunzaji wa mazingira katika kukuza maendeleo ya miji ya siku zijazo. Tathmini ya UNEP juu ya Mazingira ya Expo-2010 ililenga zile sehemu tisa za juhudi za jiji la Shanghai za kuhakikisha kutakuwepo mazingira yanayoridhisha kwenye maonyesho: tathmini ilifanyiwa kupima ubora wa hewa ya eneo la maonyesho, na katika shughuli za usafirishaji na uchukuzi, ufanisi wa matumizi ya nishati, maangamizi ya takataka ngumu, upatikanaji wa maji safi na salama, funiko la mazingira ya kijani, sehemu za jiji zilizohifadhiwa, hali ya hewa isiotangua pamoja na kufanyiwa tathmini ya hali kijumla kwenye viwanja vya Expo-2010.