Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria za kiutu za kimataifa ziliharamishwa Ghaza, imeripoti UM

Sheria za kiutu za kimataifa ziliharamishwa Ghaza, imeripoti UM

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay leo ametangaza ripoti yenye kuonyesha kulifanyika uharamishaji wa hali ya juu wa sheria ya kiutu ya kimataifa pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu, uliotukia baina ya tarehe 27 Disemba 2008 hadi Januari 18, 2009 katika eneo liliokaliwa la WaFalastina katika Tarafa ya Ghaza.

Ripoti ilisema ukiukaji mkubwa wa haki za kiutu uliendelezwa na vikosi vya Israel wakati wakitekeleza zile operesheni za mashambulizi dhidi ya Ghaza, zilizopewa jina la "Operesheni ya Kumimina Risasi". Ripoti vile vile ilizingatia ukakamavu wa Israel kutotekeleza mapendekezo ya Mahakama ya Kimataifa iliopo Hague kuhusu Ukuta uliojengwa kwenye maeneo ya WaFalastina, na vile vile kuendelea kuweka vikwazo dhidi ya watu na uingizaji wa vifaa na bidhaa zinazohitajika kunusuru maisha ya waathirika wa mashambulio ya Ghaza, ikichanganyika na vikwazo ziada kwa wakazi wa KiFalastina wa eneo la Magharibi ya Mto Jordan, hatua ambazo Pillay alisema zinaharamisha kifungu cha 33 cha Mkataba wa Nne wa Geneva juu ya hifadhi ya watu waliokaliwa kimabavu na taifa geni.