Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF imeripoti hali ya usalama itachelewesha ugawaji wa misaada ya kunusuru maisha Usomali

UNICEF imeripoti hali ya usalama itachelewesha ugawaji wa misaada ya kunusuru maisha Usomali

Taarifa ilitoka Nairobi siku ya leo ya Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) imeeleza kuwa shirika litaakhirisha kupeleka misaada ya chakula cha kunusuru maisha ya watoto 85,000, wanaoteseka na utapiamlo hatari, katika baadhi ya sehemu za majimbo ya Usomali ya kati na kusini, kwa sababu ya kukithiri kwa uhasama dhidi ya watumishi wa mashirika yanayohudumia misaada ya kihali.

Kadhalika, UNICEF imeeleza huduma za kugawa vyandaraua katika Usomali, vilivyonyunyizwa madawa, dhidi ya malaria, kwa wanawake na watoto wanaokadiriwa 100,000, zimechafuliwa na kusitishwa kwa sababu ya mapigano. Lakini kwenye yale maeneo ambayo usalama umedhibitiwa, UNICEF inasema itaendelea kupeleka misaada ya kihali inayohitajika kukidhi mahitaji ya umma waathirika nchini Usomali. UNICEF ilikumbusha kwamba kitovu cha operesheni zake, katika majengo ya UNICEF yaliopo mji wa Jowhar, Usomali ya Kati, kilitekwa nyara mnamo tarehe 17 Mei 2009 ambapo akiba kubwa ya vyakula pamoja na vifaa vya mawasiliano viliangamizwa na kupokonywa kutoka ghala za UNICEF za Jowhar. Vile vile misaada mengine ya dharura iliowekwa kwenye ghala za washiriki wanaohudumia misaada ya kiutu katika Jammame, jimbo la Juba ya Chini, vifaa na vyakula hivyo viliibiwa katika mwanzo wa mwezi Agosti. Kama inavyofahamika, Shirika la UNICEF ndio lenye kuongoza katika ugawaji wa chanjo na madawa yanayohitajika kwa mama wajawazito, na kwenye zahanati pamoja na vituo vya afya vinavyoshughulikia afya ya watoto milioni 1.2 chini ya umri wa miaka mitano na wanawake milioni 1.4 katika eneo la Kati la Usomali Kusini. Ripoti ya UNICEF imehadharisha kwamba maisha ya watoto wadogo hawa na wanawake wa eneo yatahatarishwa sana pindi UM utashindwa kuendeleza kazi zake kikamilifu na kugawa misaada ya kihali kwa umma huu muhitaji.