Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Alkhamisi Baraza la Usalama limeongeza sauti yake miongoni mwa jamii ya kimataifa na kutaka wafungwa wote wa kisiasa katika Myanmar waachiwe, ikijumuisha kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi. Kadhalika Baraza la Usalama limeeleza kuingiwa wahka juu ya hukumu ya kuongeza kifungo cha nyumbani cha miezi 18 ziada, dhidi ya Aung San Suu Kyi, ambaye sasa hivi ameshakamilisha miaka 14 ya kizuizi cha ndani ya nyumba kabla ya hukumu iliotolewa wiki hii. Kwenye risala ya Baraza la Usalama iliosomwa na Raisi wake kwa mwezi Agosti, Balozi Tom Sawers wa Uingereza ilisisitiza umuhimu wa Serikali ya Myanmar kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa, na kuisihi Serikali "kuchukua hatua zinazotakikana kuandaa mazingira yanayohitajika kuendeleza majadiliano yanayoaminika na Dauw Aung San Suu Kyi pamoja na vyama vyote husika, na pia makundi ya kikabila yaliopo Myanmar ili baadaye kuleta upatanishi wa pamoja wa taifa." Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza kwenye risala kwamba wanaunga mkono mchango wa ofisi ya KM katika shughuli za kuleta suluhu inayoridhisha katika Myanmar kwa natija za raia wote.

KM Ban Ki-moon, amenakiliwa na msemaji wa ofisi yake kukaribisha ahadi ya Serikali ya Marekani ya kujihusisha kwa nguvu zaidi na shughuli za Umoja wa Mataifa, kauli iliorudiwa kwenye hotuba ya Balozi wa Marekani katika UM, Susan Rice iliotolewa Ijumatano katika Chuo Kikuu cha New York, kwa niaba ya Serikali ya Raisi Barak Obama. Balozi wa Marekani alisema kwenye hotuba yake ya kuwa "hali njema na ustawi wa Marekani" pamoja na "masilahi yanayohusu usalama wa Marekani yenyewe" katika karne ya 21 hayatoweza kutekelezwa bila ya kutumia "chombo cha UM kuendeleza sera za Marekani na haki za watu wote." Kwa upande wake KM alisisitiza uongozi na mchango wa Marekani ni muhimu katika kuiwezesha UM kukabiliana, kwa mafanikio, na mchanganyiko wa matatizo kadha yalioselelea ulimwenguni kwa hivi sasa, ikijumlisha athari za mabadiliko ya hali ya hewa, masuala yahusuyo usalama na amani, na vile vile haki za binadamu. KM aliahidi ya kuwa ataendelea kuimarisha miradi ya kuleta mageuzi kwenye shughuli za UM, na alisema anasubiri kwa hamu kushirikiana na Marekani, pamoja na Mataifa Wanachama yote katika UM, na kuhakikisha mahitaji ya nchi wanachama yanatekelezwa kwa ufanisi na uwazi unaoridhisha.