Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa KM apongeza kuachiwa huru wahudumia misaada Usomali

Mjumbe wa KM apongeza kuachiwa huru wahudumia misaada Usomali

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah, leo ametoa taarifa yenye kupongeza kuachiwa huru kwa wahudumia misaada ya kiutu wanne pamoja na marubani wawili waliotekwa nyara miezi tisa iliopita nchini Usomali.

Wahudumia misaada ya kiutu hawa wanne, waliokuwa wakitumikia shirika lisio la kiserikali la Ufaransa linaloitwa Action Contre La Faim (Jumuiya ya Utendaji Dhidi ya Njaa) pamoja na marubani wawili walitoroshwa mwezi Novemba 2008 kutoka uwanja mdogo wa ndege katika mji wa Dusamareb, uliopo Usomali ya kati. Vile vile Ould-Abdallah alisema tusisahau kwamba kuna Wasomali kadha wengine pamoja na raia wa kigeni ambao bado wameshikwa kimateka kwenye mazingira yasiokubalika, kitendo ambacho alisisitiza ni lazima kulaaniwa na raia wote wa Usomali pamoja na jumuiya ya kimataifa. Taarifa za Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) inasema UM, mara kwa mara, hutoa nasaha kwa makundi yote nchini Usomali inayoyataka wahakikishe usalama wa wahudumia misaada ya kihali, ambao wanaendeleza operesheni za kiutu nchini mwao, ili waweze kukidhi mahitaji ya kihali kwa watu milioni 3, sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu katika Usomali, umma ambao umedhoofika zaidi kutokana na mchanganyiko wa mapigano, ukame, bei ya juu ya chakula na kuporomoka kwa thamani ya fedha za kizalendo.